Mafuriko ya ghafla na maporomoko ya ardhi, yaliyosababishwa na mvua za masika, yameua watu wasiopungua 50 na kusababisha maelfu ya watu kutoroka makazi yao nchini Bangladesh katika wiki iliyopita, mamlaka zimesema Jumapili, Julai 12.

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Na: RFI na mashirika mengine

Matangazo ya kibiashara

Kwa siku kadhaa, jeshi na walinzi wa mpaka wamekuwa wakipeleka chakula, maji ya kunywa, na vifaa vingine muhimu kwa meli kwa jamii zilizotengwa kutokana na mafuriko makubwa katika wilaya za kusini mashariki mwa nchi.

Angalau watu 50 walifariki katika wiki iliyopita katika wilaya iliyoathiriwa zaidi ya Chattogram, na 29 kati yao walifukiwa na maporomoko ya ardhi, Mkuu wa polisi katika eneo hilo, Mohammed Ziauddin ameliiambia shirika la habari la AFP, akibainisha kwamba “watu wawili bado hawajulikani walipo.” Takriban watu 35,000 wametafuta hifadhi katika vituo vinavyoendeshwa na serikali, ameongeza.

Wizara ya Usimamizi wa Maafa ilitangaza siku ya Jumamosi, Julai 11, kwamba mafuriko katika wilaya saba – Chattogram, Cox’s Bazar, Bandarban, Rangamati, Khagrachhari, Moulvibazar, na Habiganj – yamevuruga maisha ya kila siku, yakiwatenga maelfu ya familia, na kuziacha kaya 267,918 bila kupata huduma muhimu.

Uhaba wa maji ya kunywa na chakula

Mamlaka imefungua takriban makazi 4,000 kwa wakazi waliohamishwa, lakini uhaba wa maji ya kunywa na chakula unazidisha mgogoro huo. Wakazi wengi wako katika hali ngumu sana, huku nyumba zao na jiko zikiwa zimefunikwa na maji ya mafuriko. Wiki iliyopita, mvua kubwa ilisababisha maporomoko ya ardhi katika kambi ya wakimbizi ya Rohingya huko Cox’s Bazar, na kuua watu wasiopungua 15.

Wakimbizi zaidi ya milioni 1.2 wanaishi katika makazi yaliyojaa watu kwenye miteremko isiyo na miti, ambayo hufanya ardhi kuwa isiyo imara wakati wa msimu wa mvua za masika. Hali katika wilaya za kusini mashariki inatarajiwa kuboreka haraka, Sarder Udoy Raihan wa Kituo cha Utabiri na Onyo la Mafuriko aliliambia shirika la hbari la AFP siku ya Jumapili. “Lakini mvua za masika bado zinaendelea kaskazini mashariki na kaskazini mwa Bangladesh, na mafuriko zaidi yanawezekana,” aliongeza.

Bangladesh ni miongoni mwa nchi zinazokumbwa na maafa mengi zaidi duniani, huku mvua za masika za msimu zikisababisha mafuriko mara kwa mara, mmomonyoko wa mito, na maporomoko ya ardhi. Kulingana na wanasayansi, mabadiliko ya tabianchi yanaongeza marudio na nguvu ya mvua kubwa, na hivyo kuzidisha ukubwa na ukali wa majanga haya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *