Michuano ya Olimpikiya majira ya baridi 2026, imefunguliwa rasmi Februari 6-22 katika miji miwili ya Italia ya Milan-Cortina.
Hafla ya ufunguzi inafanyika Ijumaa na kujumuisha maonyesho kutoka maeneo yote ya mashindano, huku wanariadha 2,900 wakipita karibu na viwanja wanavyoshindania.
Sherehe hizo za ufunguzi zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance na Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio. Marekani inatarajiwa kuwa mwenyeji wa michezo ijayo ya majira ya joto mwaka 2028 huko Los Angeles.
Programu ya michezo hiyo iliyopewa jina la Milan-Cortina tayari imeanza siku ya Jumatano huku Marekani ambayo ni bingwa mtetezi ikichukua uongozi tayari katika baadhi ya vipengele.
Usalama waimarishwa
Kuelekea michezo hiyo, mamlaka za Italia zimeimarisha ulinzi kuelekea ufunguzi wa Michezo ya Majira ya Baridi ya Milan–Cortina, ikisambaza maelfu ya maafisa kuhakikisha usalama wa wanamichezo, watazamaji na viongozi wa dunia katika maeneo mbalimbali kuanzia Milan hadi milima ya Dolomites.
Siku moja kabla ya ufunguzi, Baraza la Waziri Mkuu Giorgia Meloni lilipitisha amri mpya ya usalama yenye masharti makali zaidi ili kukabiliana na maandamano yanayoweza kuzuka, hatua ambayo imekosolewa na baadhi ya wabunge wa upinzani wakidai inabana uhuru wa kujieleza.