Iran imesema mazungumzo ya nyuklia kati yake na Marekani yaliyofanyika nchini Oman yalikuwa mwanzo mzuri na yatendelea, wakati hofu ya kuzuka kwa vita nyingine Mashariki ya Kati ikiendelea kuongezeka.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, alisema pande zote zimekubaliana kuendelea na mazungumzo baada ya duru za awali kufanyika kwa upatanishi wa Oman mjini Muscat.
Akizungumza na televisheni ya taifa, Araqchi alisema kulikuwa na uelewano kuhusu mwelekeo wa mazungumzo yajayo, huku maamuzi ya hatua zinazofuata yakifanywa katika miji mikuu ya nchi husika.
Mazungumzo hayo yalifanyika kwa njia isiyo ya moja kwa moja, huku wajumbe wa kila upande wakikutana kwa nyakati tofauti katika kasri moja lililo karibu na uwanja wa ndege wa Muscat.
Maafisa kutoka Tehran na Washington wanatarajiwa kurejea nyumbani kwa mashauriano zaidi kabla ya kutangaza ratiba ya duru inayofuata.
Tehran yakataa kupanua ajenda ya mazungumzo
Wakati Iran ikisisitiza kuwa mazungumzo yanapaswa kuangazia tu mpango wake wa nyuklia, Marekani imedokeza kutaka ajenda ipanuliwe kujumuisha makombora ya masafa marefu na ushawishi wa Tehran kwa makundi yenye silaha katika Kanda ya Mashariki ya Kati.
Araqchi amekariri kuwa Iran haitajadili uwezo wake wa kijeshi, hususan mpango wa makombora, akisema mazungumzo yoyote yanapaswa kufanyika bila vitisho wala shinikizo.
Kwa upande wake, Washington imeweka mstari mwekundu kuhusu urutubishaji wa urani ndani ya Iran, ikitaka udhibiti mkali zaidi au kusitishwa kabisa kwa shughuli hizo.
Iran imeashiria kuwa iko tayari kuonyesha unyumbufu fulani, ikiwemo uwezekano wa kukabidhi kiasi cha urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha juu na kukubali mpango wa ushirikiano wa kimataifa.
Hata hivyo, Tehran inasisitiza kuwa kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi vilivyorejeshwa mwaka 2018 ni sharti muhimu la kufikiwa kwa makubaliano yoyote mapya.
Hofu ya vita na ongezeko la majeshi ya Marekani
Mazungumzo haya yamekuja miezi kadhaa baada ya Marekani kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran na wakati maandamano makubwa ya kitaifa yakitikisa Jamhuri hiyo ya Kiislamu.
Uwepo mkubwa wa jeshi la wanamaji la Marekani katika eneo hilo, ikiwemo meli za kivita na ndege za kivita, umeongeza shinikizo kwa Tehran huku Rais Donald Trump akionya kuwa “mambo mabaya” yanaweza kutokea iwapo hakutakuwa na makubaliano.
Nchi za Ghuba zina hofu kuwa kushindwa kwa mazungumzo kunaweza kusababisha vita vya kikanda, hasa kutokana na vitisho vya kulipiza kisasi kutoka Iran iwapo itashambuliwa.
Iran imeyaonya mataifa jirani yanayohifadhi kambi za kijeshi za Marekani kuwa yanaweza kuwa shabaha iwapo yatashiriki katika shambulio lolote.
Wachambuzi wanaeleza kuwa mafanikio ya mazungumzo hayo yatategemea uwezo wa pande zote kuvuka vihunzi vya ukosefu wa imani uliopo na kufikia mfumo wa makubaliano utakaodhibiti mpango wa nyuklia bila kuchochea mgogoro mpya wa kijeshi.