
Naibu kamanda wa Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) anayesimamia masuala ya kisiasa amesema kuwa kuoneshwa hivi karibuni kwa kombora la kisasa la masafa marefu lenye “nguvu ya uharibifu isiyo ya kawaida” ni kielelezo cha msimamo imara wa Iran wa kudumisha uwezo wake wa kujilinda.
Brigedia Jenerali Yadollah Javani alitoa kauli hiyo katika mahojiano na mtandao wa televisheni wa Lebanon, al-Mayadeen, akiashiria kombora la Khorramshahr-4, ambalo utendaji wake wa kioperesheni ulioneshwa na IRGC wakati wa uzinduzi wa “mji mpya wa makombora wa chini ya ardhi.”
Kwa mujibu wa IRGC, kombora hilo lina uwezo wa kulenga hadi masafa ya kilomita 2,000 (maili 1,242), usahihi wa kulenga wa takribani mita 30, na uwezo mkubwa wa kupenya ngome kutokana na kasi yake ya juu ya hipasoniki na uwezo wa kubadilika mwelekeo, likifikia kasi ya Mach 16 nje ya angahewa na Mach 8 ndani yake.
Javani amebainisha kuwa wapinzani wa Jamhuri ya Kiislamu wanapaswa kuchukua funzo kutokana na maendeleo hayo, akisisitiza kuwa kombora la Khorramshahr-4 ni sehemu tu ya uwezo mpana wa kijeshi wa Iran.
Akiashiria mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani yaliyofanyika Ijumaa katika mji mkuu wa Oman, Muscat amesema: “Pamoja na kuwa Iran imefika katika meza ya mazungumzo, haina nia ya kuachana na nguvu zake za kijeshi.”
Jenerali Javani amepinga wazo kwamba ushiriki wa Iran katika mazungumzo ni dalili ya udhaifu. “Hatutaki vita, lakini iwapo upande wa pili utafanya kosa, tutajibu kwa nguvu kubwa,” alisema, akiongeza kuwa timu ya mazungumzo ya Tehran imeingia katika mazungumzo ikiwa na msimamo wa nguvu.
Aidha amesema Marekani inasisitiza kujadili uwezo wa makombora wa Iran, sharti ambalo Jamhuri ya Kiislamu imelikataa. Jenerali Javani amesema kiwango cha juu cha uwezo wa kumzuia adui cha Iran kimewafanya mahasimu wake kujaribu kuinyima nchi hii uwezo wake wa kujilinda kupitia mazungumzo.
Hata hivyo, ameisitiza kuwa “nguvu ya ulinzi ya Iran lazima ihifadhiwe na kuimarishwa,” akibainisha kuwa makundi yote ya kisiasa nchini yanakubaliana juu ya kulinda uwezo wa kujihami wa taifa.
Afisa huyo aliendelea kwa kusisitiza utayari kamili wa Majeshi ya Iran kukabiliana na aina yoyote ya uchokozi.