Mkuu wa Baraza la Utawala nchini Sudan, Luteni Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, amesema kwamba hakutakuwa na amani na wale walioua, kupora na kuwafurusha makwao watu wa Sudan.

Al Burhan amesema hayo katika hotuba ya hadhara aliyoitoa katika Jimbo la Al-Jazirah, kwenye hadhira ya wenyeji, wakulima na viongozi wa Kisufi.

Kuhusu suala la makubaliano ya amani na kundi la waasi la Rapid Support Forces (RSF), Al Burhan amepuuza umuhimu wa mazungumzo yoyote na kundi ambalo amesema limefanya mauaji, uporaji na kulazimisha raia kuhama makazi yao na amepinga kabisa wazo la kurudi kwenye meza ya mazungumzo na wale aliowaelezea kama adui.

Kiongozi wa Baraza la Utawala nchini Sudan ametoa wito wa wazi kwa watu wenye silaha aliowataja kama waliopotoshwa na kujiunga na RSF, akiwataka wakabidhi silaha zao na warudi nchini. Amesisitiza kwamba mlango wa msamaha bado uko wazi, na kwamba Sudan ni nchi yao; hivyo wanapaswa kuachana na wale wanaowaongoza kwenye maangamizi.

Tangu waasi wa RSF waanzishe vita dhidi ya serikali ya Sudan mwezi Aprili 2023, maelfu ya watu wameuawa na wengine  zaidi ya milioni 12 wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi, huku mikoa kadhaa ikikumbwa na njaa na uhaba wa chakula.

Mwezi uliopita wa Januari, Nazhat Shameem Khan, Naibu Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), amelituhumu kundi la Rapid Support Forces (RSF) kuwa limechimba makaburi ya halaiki ili kuficha “uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu” uliofanywa katika eneo la Darfur, magharibi mwa Sudan.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *