
Iran na Marekani zimekubaliana “kuendelea na mazungumzo yao,” Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi alisema siku ya Ijumaa baada ya duru ya kwanza ya mazungumzo yaliyofanyika Oman katika kile alichokielezea kama mazingira “chanya”.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Ijumaa amesifu mazungumzo “mazuri” yanayoendelea na Iran, kufuatia kikao cha mazungumzo nchini Oman, akisema kwamba mazungumzo yataendelea “mapema wiki ijayo.”
“Pia tulikuwa na mazungumzo mazuri sana na Iran. Iran inaonekana kuwa na hamu kubwa ya kufikia makubaliano,” rais wa Marekani, ambaye alituma kikosi kikubwa cha jeshi la majini Ghuba, aliwaambia waandishi wa habari ndani ya ndege ya rais ya Air Force One.
“Matokeo ya leo na Iran yalikuwa mkutano mmoja. Tutakutana tena mapema wiki ijayo,” aliongeza.
“Katika mazingira chanya sana, mawazo yetu yalibadilishwa na maoni ya upande mwingine yakawasilishwa kwetu,” Bw. Araghchi aliambia televisheni ya taifa ya Iran. Aliongeza kuwa pande zote mbili “zilikubaliana kuendelea na mazungumzo, lakini kwamba taratibu na ratiba zitaamuliwa baadaye.”
Mazungumzo kuhusu suala la nyuklia
Kwa hivyo, tishio la vita linapungua kidogo, ingawa wiki moja tu iliyopita, Rais Trump aliitishia Iran kwa mashambulizi makali zaidi kuliko yale ya mwezi Juni mwaka uliyopita, anaripoti mwandishi wetu huko Tehran, Siavosh Ghazi. Tehran imekataa kujadili mpango wake wa makombora ya balestiki na uwezo wake wa kijeshi na ulinzi, pamoja na sera yake ya kikanda na usaidizi kwa makundi kama vile Hezbollah, Houthi huko Yemen, Hamas, na makundi ya Kishia nchini Iraq.
“Tunajadili tu suala la nyuklia na Marekani,” waziri wa mambo ya nje wa Iran alitangaza siku ya Ijumaa baada ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na ujumbe wa Marekani.