
Sadeq Ashtari, kiongozi wa genge la kigaidi aliyepewa mafunzo na shirika la ujasusi la utawala wa kizayuni wa Israel Mossad kwa ajili ya kuendesha “vita vya mitaani” ameangamizwa katika mapigano na vikosi vya intelijensia vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kwa mujibu wa ripoti, mapigano hayo yamepelekea kukamatwa pia wanachama waliobaki wa kundi hilo la kigaidi.
Vyombo kadhaa vya habari hapa nchini vimeripoti kuwa Ashtari, ambaye alipatiwa mafunzo hayo na maafisa wa Mossad huko Erbil, Kurdistan ya Iraq, aliongoza shambulio kwenye kituo cha polisi katika eneo la Tehranpars la mji mkuu Tehran mnamo mwezi uliopita wa Januari.
Duru hizo za habari zimebaini kuwa eneo lililolengwa na magaidi hao mapema mwezi Januari ni Kituo cha Polisi cha 126 kilichoko katika eneo la Tehranpars.
Kituo hicho kilishambuliwa na genge hilo la kigaidi lililoongozwa na Ashtari wakati wa machafuko ya umwagaji damu yaliyozuka maeneo mbalimbali nchini ambayo yaliratibiwa na kuungwa mkono na Marekani na utawala wa kizayuni Israeli, lengo likiwa ili kuyageuza maandamano ya amani ya wananchi ya kulalamikia hali ngumu ya uchumi kuwa wimbi la machafuko.
Hata hivyo, njama hiyo ilkabiliwa na mara moja na vikosi vya intelijensia na vya usalama vya Iran, ambavyo viliwazingira vinara wa magenge ya kigaidi na kunasa maficho ya silaha zao, zikiwemo zilizokuwa zimekusudiwa kuingizwa kwenye mji mkuu Tehran.
Shakhsia kadhaa mashuhuri wa Marekani, wamethibitisha wao wenyewe jinsi pande za nje zilivyoshika katika machafuko yaliyozuka Iran, ambapo mkuu wa zamani wa shirika la ujasusi la nchi hiyo CIA, Mike Pompeo, amekiri hadharani kuhusika kwa Mossad katika machafuko hayo.
Maafisa wa Iran wameshasisitiza mara kadhaa kwamba, wakati wanaendelea kushughulikia changamoto za kiuchumi za ndani, vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu vitatoa jibu kali na madhubuti kwa vitisho vyovyote vilivyo dhidi ya usalama, mamlaka ya kujitawala, na ardhi ya nchi hii…/