Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Abbas Araghchi ameonya kwamba, iwapo Marekani itashambulia Iran, vituo vya kijeshi vya nchi hiyo katika eneo la Asia Magharibi navyo vitashambuliwa.

“Ikiwa Marekani itaishambulia Iran, tutavishambulia vituo vya Marekani katika eneo hili kwa sababu ndivyo vinavyoweza kufikiwa,” ameeleza bayana Araghchi alipohojiwa na vyombo vya habari kando ya Jukwaa la 17 la Al Jazeera lililofanyika katika mji mkuu wa Qatar, Doha siku ya Jumamosi.

Amebainisha wazi kwamba Tehran haitashambulia ardhi ya nchi jirani, bali itashambulia pale tu vilipo vituo vya kijeshi vya Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekumbusha kuwa, Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu vimejiandaa kikamilifu kutoa jibu kali na madhubuti wakati wowote ule kwa hatua yoyote ya kiuadui.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran ameeleza kwamba Jamhuri ya Kiislamu imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kwamba mpango wake wa makombora hauwezi kujadiliwa, kwa sababu unahusiana na ulinzi tu na kwa hiyo hauwezi kufanyiwa mazungumzo yoyote.

Halikadhalika, Araghchi amesema, Iran ina haki isiyoweza kufutwa ya kurutubisha urani, na kwamba mchakato huo inapasa uendelee; na akasisitiza kuwa hata mashambulizi ya kijeshi yaliyofanywa hayakuweza kufuta uwezo wa Iran…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *