z

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images

    • Author, Khanyisile Ngcobo
    • Akiripoti kutoka, Johannesburg
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Mfalme wa Zulu Afrika Kusini, amezua gumzo baada ya kutoa matamshi ya kuwadhalilisha raia wa kigeni, na kuwataka waondoke nchini humo.

Mfalme huyo alitoa semi hizo wakati ambapo alitarajiwa kutoa hotuba itakayowatuliza watu wanaowapinga raia wa kigeni katika wilaya yake ya KwaZulu-Natal.

Onyo: Taarifa hii ina mmaelezo ambayo yanaweza kukukera

Misuzulu kaZwelithini alikuwa akiwahutubia wafuasi wake katika eneo ambalo wapiganaji 20,000 wakizulu waliwashinda wanajeshi 1,800 wa Uingereza miaka 147 iliyopita, chini ya mlima wa Isandlwana .

Vita vya Isandlwana, ambavyo vilitokea wakati jamii ya Wazulu ilikuwa inawapinga Waingereza, ni jambo ambalo Wazulu hujivunia pakubwa; kuwa walipigana dhidi ya jeshi la Uingereza na kushinda vita hivyo.

Hasira ya mfalme Misuzulu na watu wake, ameilekeza kwa wahamiaji kutoka mataifa jirani kama Lesotho, Msumbiji na Zimbabwe ambao wameingia Afrika Kusini kutafuta nafasi za ajira.

Kulingana na takwimu, taifa hilo ni nyumbani kwa takriban wahamiaji million 2.4, ambao ni 4% ya idadi ya watu nchini humo.

Mfalme huyo mwenye umri wa miaka 51, hakuchochea vita ila alisema “kwerekwere”,neno la kuwadunisha wahamiaji na

kuwataka waondoke na mabegi yao hata kama wana uhusiano na raia wa Afrika Kusini na hata kuzaa Watoto.

“Lazima tukae chini tujadili hili, hata kama baba ya binamu yangu ni ‘kwerekwere’,ataondoka na kumwacha mtoto. ” Alisema mfalme huyo.

A enactment in 2023 of the Battle of Isandlwana with Zulu warriors with shields and spears bearing down on British soldiers with guns in red jackets and white helmets, several of whom have fallen to the ground.

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images

Baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii, waliweza kubaini kiini cha kauli zake, ikizingatiwa kwamba mama yake mzazi anatokea Eswatini, na mmoja wa wake zake anotokea ufalme jirani.

Ila mitazamo ya chuki kama hii imekuwa changamoto Afrika Kusini, na zimesababisha kuzuka kwa vita, na kauli zake zinaendana na alizowahi kutoa marehemu babake Goodwill Zwelithini, ambapo mwaka wa 2015 aliwataka wahamiaji kupakia mabegi yao na kuondoka.

Baadaye alijaribu kurekebisha kauli zake na kudai alinukuliwa vibaya, ila shirika la kutetea haki za kibinadamu nchini humo ilisema kauli zake zilikuwa za ‘kuumiza na zenye madhara.”

Muongo mmoja baadaye, chuki dhidi ya wahamiaji inatumiwa kama kipengele cha siasa, wengi wakiamini wahamiaji wanachukua nafasi zao za ajira, na wananufaika na mfumo wa huduma za serikali za Afrika Kusini kuliko raia wa taifa hilo.

Viwango vya ukosefu wa ajira Afrika Kusini bado ni vya juu kote duniani kwa 33%.

Hiki ni kitu ambacho vyama vya upinzani kama uMkhonto weSizwe (MK), kinachoongozwa na rais wa zamani wa taifa hilo Jacob Zuma, ambaye anawafuasi wengi kutoka KwaZulu-Natal, anatumia semi sawia za kutaka wahamiaji ambao hawana vibali sahihi kufukuzwa nchini humo.

Hii imechangia kuzuka kwa makundi yanayopinga wahamiaji nchini humo kama Dudula na March on March, ambao wamekuwa wakitaka serikali kuwafukuza wahamiaji kutoka taifa hilo. “Dudula” inamaanisha ‘kuondoa kitu kwa nguvu’ katika lugha ya Kizulu.

Kampeni yao ya mwisho ilikuwa siku chache tu kabla ya hotuba ya mfalme wa Zulu, na kabla ya kuanza kwa mwaka mpya wa masomo.

Waandamanaji wenye ghadhabu walivamia shule moja ya msingi katika mji wa Durban eneo la KwaZulu-Natal, na kudai kuwa 90% ya wanafunzi ni watoto wa wahamiaji.

Maandamano hayo yalisababisha wazazi kuitwa shuleni kuwachukua wanao, huku polisi wakitumwa kushika doria katika lango la shule ya msingi ya Addington.

Mamlaka za eneo hilo zilikemea vikali viongozi wa maandamano hayo ambayo yalikuwa yakiungwa mkono na chama cha MK.

Tukio hilo lililazimu idara ya elimu kutoa takwimu za kitaifa zinazoonyesha kuwa wanafunzi wa kigeni 253,618 apo katika shule za msingi za umma za Afrika Kusini ambao ni 1.8% ya wanafunzi wote nchini humo. Kati ya hao 14,929, wako katika shule za msingi za KwaZulu-Natal.

Wataalam wanasema kuwa watoto wote walioko Afrika Kusini wanahaki kisheria kupata elimu, bila kuzingatia uraia wao au vibali walivyonavyo.

A woman in a white Operation Dudula T-shirt and wearing camouflage cap and scarf smiles as she participates in a demonstration by the anti-migrant group. Others are similarly dressed and a South African flag can be seen.

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images

Kufuatia tukio hilo la maandamano katika shule ya msingi ya Addington, mfalme Misuzulu, alisema atazungumzia swala hilo.

Mfalme huyo hana nguvu kisiasa,ila ana ushawishi miongoni mwa wakaazi wa KwaZulu-Natal, ufalme huo bado unafadhiliwa na walipakodi wa Afrika Kusini.

Dkt Vusumusi Sibanda, wakili wa haki za kibinadam na mtaalam wa maswala ya diaspora, alisema kauli hizi zinatia wasiwasi na ni ya kusikitisha

“Mfalme anaheshimiwa na watu wengi ikiwemo raia wa kigeni, na anafaa kuashiria hilo,” Sibanda aliiambia BBC

Lizette Lancaster,ambaye anafanya kazi na taasisi ya Security Studies think-tank Afrika Kusini, amesema kuwa “kauli za mfalme zinachochea semi za kupinga wahamiaji na anafaa kukashifiwa vikali. “

Aliongezea kuwa ingawa sheria ya Afrika Kusini inawalinda waandamanaji, semi za kuchochea kufukuzwa kwa wahamiaji zinafaa kupingwa.

Kiongozi wa kundi la March on March, Jacinta Ngobese Zuma, kwa sasa anakumbwa na shtaka la kuzua vurugu katika shule ya msingi Addington.

Riot police with shields confront an angry man from Operation Dudula in a camouflage top and cap. One of the officers is pointing a finger at him.

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images

Mada nyingine ambayo ilioibuliwa na mfalme ni kutoa jina ‘Natal’ kutoka kwa KwaZulu-Natal akisema anafuata matamanio ya babake.

“Tunahitaji kutoa hili jina ‘Natal’. Hii ni KwaZulu kwa hivyo sijui kwanini tunatumia hii jina Natal. Alisema mfalme.

Kabla ya 1994, na kumalizika kwa mfumo wa ubaguzi wa rangi, wilaya ya sasa ya KwaZulu-Natal, iligawanywa mara mbili.

KwaZulu ilitengwa kuwa eneo la makaazi linalojisimamia la jamii ya waZulu, ambayo ilikuwa ndani ya Wilaya ya Natal.

Baada ya uhuru na kuja kwa utawala wa demokrasia na Nelson Mandela, wilaya hizo mbili zilirudishwa kuwa moja na majina hayo kuunganishwa.

Katika miongo mitatu iliyopita, majina ya miji na barabara zimebadilishwa na kupewa majina ya kiasili na mashujaa waliopambana na ubaguzi wa rangi.

Kuna hofu kuwa kubadilishwa kwa jina la KwaZulu-Natal, huenda ukaleta hali ya upekee ambayo huenda ikaleta matatizo katika taifa hilo lenye makabila mengi. Afrika Kusini inalugha 11 za kitaifa.

Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *