Mohammad Bagher Ghalibaf alipuuza tishio la Donald Trump la kuanzisha tena mashambulizi dhidi ya Iran.

Chanzo cha picha, Reuters

Mazungumzo kati ya Marekani na Iran ya kufikia makubaliano ya mwisho ya kumaliza vita yanatarajiwa kuendelea usiku kucha nchini Uswisi, afisa mwandamizi wa Marekani anayeshiriki katika mazungumzo hayo amesema.

Mazungumzo hayo yalianza Jumapili, kufuatia makubaliano ya wiki iliyopita ya kufikia suluhu ndani ya siku 60.

Jumapili usiku, mwanadiplomasia huyo wa Marekani alisema kwamba majadiliano yalikuwa yakijikita katika kufafanua baadhi ya ujumbe zilizokuwa hazieleweki kutoka Iran kuhusu kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz, utekelezaji wa usitishaji mapigano kusini mwa Lebanon, pamoja na baadhi ya vipengele vya makubaliano ya nyuklia.

Mapema, Rais wa Marekani, Donald Trump, alikuwa ametishia kuishambulia Iran ikiwa haitaisimamisha Hezbollah huku mapigano kati ya kundi hilo na Israel yakiendelea nchini Lebanon. Iran ilipuuzilia mbali onyo hilo, ikisema iko tayari kupigana.

Afisa huyo alisema ujumbe wa pande zote mbili, ambao unakutana katika mji wa Lucerne nchini Switzerland, utatumia matokeo ya mazungumzo ya leo kama msingi wa mazungumzo ya kiufundi yatakayoendelea.

Makubaliano ya awali ya wiki iliyopita yanajumuisha ahadi ya kufikia makubaliano ya mwisho ndani ya siku 60, pamoja na kusitishwa kwa mapigano katika maeneo yote ya mzozo, ikiwemo Lebanon, na kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz.

Hata hivyo, tangu wakati huo kumeshuhudiwa kuongezeka kwa mapigano kati ya Hezbollah na majeshi ya Israel kusini mwa Lebanon, pamoja na mashambulizi ya anga ya Israel ambayo wizara ya afya ya Lebanon imesema yamesababisha vifo vya raia kadhaa, wakiwemo wanawake na watoto.

Kuongezeka huko kwa mzozo kuliipelekea Marekani kutangaza usitishaji mpya wa mapigano kati ya Israel na Hezbollah siku ya Ijumaa.

Lakini mapigano na mashambulizi ya anga yaliyoendelea yaliifanya Iran kutangaza Jumamosi kwamba imeufunga Mlango-Bahari wa Hormuz, ingawa takwimu za ufuatiliaji wa meli zinaonesha kuwa vyombo vya majini vimeendelea kupita katika njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani.

Unaweza kusoma;

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *