TABORA: WATU sita wa familia moja, wakazi wa Kijiji cha Ulamba, Kata ya Kalunde, Manispaa ya Tabora mkoani Tabora wamenusurika kifo baada ya kupigwa na radi iliyoambatana na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia jana.
Tukio hilo limesababisha watu hao kupata majeraha katika miili yao huku nyumba waliyokuwa wakilala ikiwaka moto na kuteketeza baadhi ya mali zilizokuwemo ndani.
Wakizungumza baadhi ya wanafamilia walionusurika akiwemo Kulwa Yasin na Dotto Yasin walisema walishuhudia ngurumo kali ya radi na mara baada ya kutoka nje waliona moto ukiwaka juu ya paa la nyumba hiyo.
Kulwa alisema hali hiyo iliwalazimu kuanza kuwatoa majeruhi waliokuwa ndani ya nyumba ambao walikuwa wamepoteza fahamu na kuungua katika sehemu mbalimbali za miili yao.
Kwa upande wao, baadhi ya majirani akiwemo Ernest Sitma walisema walipofika eneo la tukio walikuta majeruhi tayari wametolewa nje ya nyumba huku nyumba ikiendelea kuteketea kwa moto.
Alisema walijitahidi kuuzima moto huo bila mafanikio, sambamba na kutoa huduma ya kwanza kwa majeruhi hao kabla ya kukimbizwa hospitalini.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Ulamba, Abdallah Kagusi alitoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari hususani katika kipindi hiki cha mvua.
Aliomba serikali pamoja na wadau kujitokeza kusaidia familia hiyo ili irejee katika maisha na makazi yake ya kawaida. Hata hivyo, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete, Swaumu Kimaro alithibitisha kuwapokea majeruhi hao sita na kusema kuwa wanaendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo, huku hali zao za kiafya zikizidi kuimarika.
