KOCHA wa Simba, Steve Barker amepiga mkwara mzito akisema kikosi hicho ni kweli kimekuwa na msimu mbaya katika michuano ya kimataifa, lakini hatarajii hilo kujitokeza katika michuano ya ndani ikiwamo Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA).

Kwa msimu wa tano mfululizo sasa Simba inasaka taji la kwanza la michuano ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho kutokana na Yanga kutawala kwa misimu minne mfululizo iliyopita, huku katika michuano ya CAF msimu huu imekosa kwa mara ya kwanza kukata tiketi ya kwenda robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa hatua ya makundi tangu msimu wa 2018-2019.

Simba iliyotoka kulazimishwa sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Petro Atletico ya Angola na kuiacha iendelee kukaa mkiani mwa Kundi D ikiwa na pointi mbili tu baada ya kuchea mechi tano na sasa inasubiri kukamilisha ratiba ya michuano hiyo ya CAF dhidi ya Stade Malien ya Mali wikiendi hii.

Mbali na mechi za Ligi ya Kombe la Shirikisho, Simba pia ina kibarua cha kusaka taji la michuano ya Kombe la Muungano 2026 baada ya kulikosa lile la Kombe la Mapinduzi 2026 lililochukuliwa na Yanga iliyoifunga Azam FC katika fainali iliyopigwa Januari 13 mwaka huu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Barker amesema inawezekana Simba ikawa na msimu mbaya katika Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini bado wana nguvu kubwa kupigania mataji ya ndani.

Amesema Simba ina timu imara ambayo imejengwa upya na baada ya muda mchache watakuwa na kikosi bora kitakachorudisha heshima ya mashabiki wa klabu hiyo.

“Wakati huu hatutaki kuendelea kuangusha pointi kwenye mashindano tunayoshiriki ili kupigania mataji  yaliyosalia, ninavutiwa na namna wachezaji wanavyoimarika siku hadi siku,” amesema Barker na kuongeza;

“Kushindwa kwetu huku kunatupa nafasi ya kusaka mataji ya mashindano mengine ikiwemo Ligi Kuu, hivyo hii ni fursa ya kujiona upya.

“Simba ni timu ambayo inaendelea kujengwa, hivyo wachezaji wakipata muda mchache zaidi na nguvu zikielekea kwenye kusaka mataji yaliyosalia, naamini tutafanikiwa.”

Kocha huyo aliyetua Msimbazi mwishoni mwa mwaka jana akitokea Stellenbosch ya Afrika Kusini aliongeza kwa kusema: “Malengo ya Simba sio kimataifa pekee, pia na ligi ya ndani kuhakikisha tunavunja rekodi ya wapinzani wetu, hivyo kumaliza hapa nguvu zote zinahamia huko, kwa hiyo tumejipanga.”

Ikumbukwe kuwa, Simba haijabeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu minne mfululizo, huku Yanga ikitawala muda wote huo na hivy kumpa kazi kocha Barker kusahihisha makocha kwa kurejesha mataji hayo iliyokuwa ikiyashikilia kwa misimu minne kabla ya Yanga kupindua meza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *