Marekani. jinsi mambo yanavyokenda katika ulimwengu wa muziki wao, ilikuwa ni wazi kabisa kuwa muda si mrefu Kendrick Lamar, 38, atakuja kupindua utawala wa muda mrefu wa Jay Z, 56, katika tuzo za Grammy.
Lamar, mkali wa kibao cha Not Like Us (2024), katika tuzo za 68 za Grammy 2026 zilizotolewa hivi karibuni huko Los Angeles, Marekani, aliandika rekodi kama rapa aliyeshinda tuzo hizo mara nyingi zaidi.
Alishinda vipengele vitano kati ya tisa alivyokuwa akiwania msimu huu, na hivyo kufikisha tuzo 27 za Grammy akimpita mwanzilishi wa Roc-A-Fella na bilionea wa kwanza katika rap, Jay Z mwenye tuzo 26.
Mafanikio hayo yalionekana wazi tangu msimu uliopita ambapo Lamar alishinda tuzo tano za Grammy 2025, na kumfanya kufikisha tuzo 22, huku wakati huo akiendelea kutamba na albamu yake ya sita, GNX (2024).
Albamu hiyo ilitoka Novemba 22, 2024 ikiwa tayari muda wa kuwasilisha kazi kwa Grammy 2025 umeshapita, hivyo ikabidi ingoje kuona kama itapenya kuwania Grammy 2026, nafasi ambayo imekuja kupatikana.
Kwa namna ilivyopelewa kwa kishindo katikati ya bifu zito la Lamar na Drake ambalo lilikuwa limepamba moto wakati huo, tayari ilitoa picha ya kile kitakachokuja kutokea Grammy 2026 na hatma ya rekodi ya Jay Z.
Lamar ambaye majarida kama Billboard na Vibe yanamtaja kama rapa bora namba mbili duniani kwa muda wote, ndiye mtayarishaji mkuu wa albamu hiyo kwa kushirikiana na Dave Free.
PGLang na Interscope Records ndio wameisimamia ikiwa ni albamu yake ya kwanza tangu kuachana na lebo za Top Dawg Entertainment na Aftermath Entertainment alizofanya nazo kazi kwa miaka mingi.
Utakumbuka Lamar alitambulika zaidi kupitia albamu yake ya pili, Good Kid, M.A.A.D City (2012) ikiwa ni baada ya kurekodi na Dr Dre chini ya Aftermath Entertainment, lebo iliyowatoa kina 50 Cent, Eminem na kadhalika.
Sasa wiki moja baada ya kuachiwa kwa GNX (2024), mtandao wa Top Of The Charts uliripoti kuwa albamu hiyo ilisikilizwa (streams) mtandaoni kati ya mara milioni 350 hadi 400. Hivyo ikaweka rekodi kama albamu ya Hip Hop iliyosikilizwa zaidi ndani ya wiki moja kwa mwaka 2024, sawa na ile ya Drake, For All the Dogs (2023) ambayo ilisikilizwa mara milioni 514 pindi ilipotoka Oktoba 6, 2023.
Lamar alifanya hivyo ikiwa ni mwezi mmoja baada ya kushinda tuzo nane za BET Hip Hop 2024 akiwa ndiye msanii aliyefanya vizuri zaidi, huku ngoma yake, Not Like Us (2024) ukishinda vipengele vitatu. Hivyo kufanya vizuri kwa GNX hakukuonyesha tu kukubalika kwake kwenye tasnia ya muziki duniani, bali pia kuimarika kwa uwezo wake wa kufikia mafanikio ya kibiashara katika mfumo rasmi.
Wakati akiendelea kutamba na albamu hiyo, ndipo alitumbuiza show ya Super Bowl 2025 ambapo show yake ilivutia watazamaji milioni 126 ikiwa ni ongezeko la asilia 2 kutoka msimu wa 2024.
Kulingana na FoxSports, hadi sasa show hiyo imetamwa na watu milioni 133.5 ikiwa ndio namba moja, ikizipita show za Usher (2024) iliyopata watazamaji milioni 123.4, na ile ya Rihanna 2023, watazamaji milioni 121. Hii ilionyesha ni kwa namna gani ushawishi wa Lamar katika muziki umezidi kukua ukilinganisha na Jay Z ambaye amekuwa kimya kimuziki kwa miaka mingi bila kutoa kazi yoyote.
Kutokana na hilo, ni wazi Lamar alikuwa ana nafasi ya kuifikia rekodi ya Jay Z ukizingatia tayari alikuwa na albamu (GNX) inayofanya vizuri na ndio iliyokuja kushinda Grammy 2026 kama Albamu Bora ya Rap.
Katika kipengele hicho Lamar aliwashinda wasanii wenzake kama Clipse, Pusha T & Malice (Let God Sort Em Out), GloRilla (Glorious), JID (God Does Like Ugly) na Tyler, The Creator (Chromakopia).
Ikumbukwe tuzo za Grammy zilianza kutolewa hapo Mei 4, 1959, wakati huo zikifahamika kama Gramophone Awards, huku lengo lake kuu likiwa ni kutambua mafanikio katika tasnia ya muziki duniani.
Hadi sasa, mke wa Jay Z, Beyonce Knowles, mwanachama wa zamani wa kundi la Destiny’s Child, ndiye mwanamuziki aliyeshinda tuzo nyingi zaidi za Grammy duniani kwa muda wote, akishinda mara 35.
Msimu uliopita alishinda kipengele cha Albamu Bora kwa mara ya kwanza baada ya kuwania mara nne bila mafanikio. Ushindi huo uliletwa na albamu yake ya nane, Cowboy Carter (2024) yenye nyimbo 27 huku akishirikisha wakongwe kibao akiwemo Dolly Parton.