Arusha. Sekta ya ujenzi nchini imefanikiwa kuanzisha na kutekeleza jumla ya miradi 81 ya miundombinu yenye thamani ya zaidi ya Sh500 bilioni ndani ya siku 100 za uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Hayo yamesemwa jana Jumapili Februari 8, 2026 na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha kuhusu tathmini ya mafanikio ya siku 100 za Rais Samia katika sekta hiyo.

Ulega amesema fedha hizo zimetumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ujenzi na ukarabati wa barabara, madaraja, vivuko, majengo ya watumishi pamoja na uwekaji wa alama na taa za barabarani.

“Ndani ya miradi 81 tuliyoianzisha, miradi 40 tayari imekamilika na mingine inaendelea. Miradi itakapokamilika, Rais Samia atafungua kwa kuchagua mmoja kuwakilisha mingine,” amesema.

Waziri huyo ametoa onyo kali kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya serikali, akiwataka kuacha uzembe, akisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaoshindwa kutimiza wajibu wao kwa wakati.

“Mkandarasi ukiomba kazi, ukalipwa fedha za wananchi halafu unazembea, hatua kali za kisheria zitachukuliwa. Serikali haitasita kuvunja mikataba na kufungua mashtaka, ikiwemo ya uhujumu uchumi, pale itakapobainika kuna uzembe au matumizi mabaya ya fedha,” amesema.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega akisalimiana na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari.

Ametoa mfano wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Kyela mkoani Mbeya ulioanza mwaka 2024, ambapo mkandarasi alitakiwa kufikia utekelezaji wa asilimia 50, lakini hadi mwaka jana alikuwa amefikia asilimia tano pekee, licha ya kulipwa zaidi ya Sh8 bilioni.

Amesema ukaguzi wa matumizi ya fedha umeanza na endapo uzembe utathibitika, mkataba utavunjwa na hatua za kisheria kuchukuliwa.

Ulega amebainisha kuwa serikali inachukua tahadhari kubwa katika kusimamia hatua hizo ili kuepuka kuingia hasara ya kulipa fidia kutokana na mashauri ya kisheria au uvunjaji wa mikataba bila kufuata taratibu.

Amesema wizara inaongeza nguvu katika ufuatiliaji na usimamizi wa karibu wa miradi, hususan barabara, madaraja na vivuko, ili kuhakikisha miundombinu hiyo inazingatia viwango vinavyokabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Mwaka jana tulitenga zaidi ya Sh100 bilioni kwa ajili ya kukarabati miundombinu iliyoharibiwa na mvua na mafuriko. Sasa tumeongeza usimamizi ili miradi iwe imara na kuepuka gharama za marekebisho ya mara kwa mara,” amesema.

Akijibu hoja kuhusu miradi mingi kutekelezwa na wakandarasi wa kigeni, Ulega amesema serikali imefanya maboresho kwa kutoa kipaumbele kwa wakandarasi wa ndani kwenye miradi isiyozidi Sh50 bilioni.

“Kati ya miradi 81, miradi 60 inatekelezwa na wakandarasi wazawa na 21 na wakandarasi wa kigeni. Watanzania wasiwe na hofu, bali wachangamkie fursa za kuomba zabuni pindi matangazo yanapotolewa,” amesema.

Ameeleza kuwa miradi yenye thamani ya zaidi ya Sh50 bilioni mara nyingi hufadhiliwa na mifuko ya kimataifa, ambayo masharti yake yanahitaji zabuni kutangazwa kimataifa, hali inayowapa changamoto baadhi ya wakandarasi wa ndani.

Hata hivyo, amesema serikali inasisitiza angalau asilimia 10 ya kazi katika miradi hiyo kutekelezwa kwa ushirikiano na wakandarasi wazawa.

“Tunalenga kuhakikisha fedha nyingi zinaendelea kubaki ndani ya nchi kupitia manunuzi na matumizi, badala ya kuendelea kutoka nje,” amesema.

Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dk Charles Msonde, amesema mkutano huo ulilenga kuwajulisha wananchi hatua zinazochukuliwa na serikali kuhakikisha huduma za miundombinu zinaboreshwa na kutolewa kwa wakati.

Kwa upande wake, mkazi wa King’ori wilayani Arumeru, Joseph Laizer, amesema utoaji wa taarifa kwa wananchi ni muhimu katika kupunguza migogoro kati ya serikali na wananchi, hasa pale wanapodhani hakuna kinachofanyika katika maeneo yao.

Ametoa wito kwa viongozi wa serikali kuanzisha majukwaa ya mara kwa mara ya kutoa taarifa za maendeleo na miradi inayopangwa, pamoja na kuwapa wananchi fursa ya kuuliza maswali kuhusu utekelezaji wa ahadi za maendeleo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *