Dar es Salaam. Katika misimu ya nyuma, viwanja vya soka nchini vilikuwa sehemu ya shamrashamra na mikusanyiko mikubwa ya mashabiki.

Mechi za Ligi Kuu Bara zilikuwa zikivuta umati mkubwa, wakati michezo ya kimataifa ilikuwa ikigeuka tukio la kitaifa kwa mashabiki kusafiri kutoka mikoa mbalimbali.

Katika miaka ya karibuni, mashabiki walizoea kuona viwanja vikigeuka sehemu za matukio makubwa, matamasha kama Simba Day na Siku ya Mwananchi ya Yanga yaliweka viwango vipya vya burudani.

Matamasha hayo yakichanganya muziki, maonyesho ya wasanii, uwasilishaji wa kisasa, na shughuli mbalimbali zinazowafanya mashabiki kufika mapema na kugeuza uwanja kuwa sehemu ya mtoko huku wakitambiana katika ujazaji wa uwanja wa watu 60,000.

Mbali na tamasha, hata kwenye mechi za kimataifa ilikuwa sehemu ya kuongeza hamasa ya kujaza uwanja kwa watani wa jadi wa Simba na Yanga kila mmoja akimtambia mwenziwe nani kaingiza watu wengi ambapo inatoa hasira kwa mpinzani kuongeza ubunifu.

Msimu wa 2025-2026, umeonyesha mabadiliko makubwa, mashabiki wamepungua kwa kiwango kinachoonekana wazi, hata kwenye mechi ambazo zamani zilikuwa zikiamsha hasira ya ushindani.

Kwanini mashabiki wamepungua?

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Azam FC, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ amesema: “Mbali na mpira kuonyeshwa kwenye TV, ushabiki wetu ni mdogo, watu wengi ni mashabiki wa matokeo. Timu ikipata matokeo, wanafika, lakini mambo yakiwa magumu, mashabiki hupungua sana.

“Kwenda uwanjani ni safari ngumu, gharama ni nyingi, foleni ni kubwa, na viwanja vingi viko mbali na makazi ya mashabiki. Hata ukifika, kuna changamoto nyingi za kuzunguka eneo la uwanja.”

Amesema mazingira hayo huwafanya mashabiki wengi kubaki nyumbani ambako wanaweza kutazama mchezo kwa urahisi bila gharama kubwa.

Sababu nyingine amesema kutokuwepo kwa wachezaji wenye majina makubwa ambao huibua hisia na hamasa kwa mashabiki pia kumechangia kupungua kwa watu viwanjani.

“Kweli ukiwa na majina makubwa kwenye timu, mashabiki huja kwa wingi. Sasa hivi majina yamepungua, na hili nalo limeathiri hamasa,” amesema.

Amesema kwa sasa wanachoamini kinaweza kuleta mabadiliko ni kuhakikisha timu inashinda na kuongeza ubora wa kikosi.

“Nguvu yetu kubwa ipo kwenye timu, tukishinda tukawa na wachezaji wenye mvuto, mashabiki watarudi viwanjani. Hiyo ndiyo sehemu tunayoweza kuingilia kwa sasa,” amesema.

Zaka za Kazi amesema Azam itaendelea kuwekeza kwenye kikosi ili kurejesha morali na hamasa ya mashabiki wanaotaka kuona burudani yenye ubora.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema klabu hiyo inatambua kupungua kwa hamasa ya mashabiki kuhudhuria mechi za timu hiyo, hususan zile za kawaida na imeanza kuchukua hatua madhubuti kurejesha nguvu ya ushiriki wa mashabiki uwanjani.

“Ni kweli hamasa imepungua, mashabiki wengi wanafuatilia mpira kupitia TV, mechi ikiendelea, mijadala mitandaoni inakuwa mikubwa kuliko idadi ya watu uwanjani. Hata mechi ikimalizika, gumzo linakuwa kubwa huko mitandaoni,” amesema Kamwe.

“Tunalishughulikia, tunataka mashabiki warudi uwanjani kwa wingi. Tunashukuru wote wanaotupa mrejesho na tunafanya kazi kwa pamoja,” amesema.

Naye, Ofisa Habari wa KMC, Khalid Chukuchuku, amesema upangaji wa viingilio kwa baadhi ya mechi unachangia kwa kiasi kikubwa kwa viwanja kutokujaa ikiwepo cha KMC Complex kwa sababu wanaofika uwanjani ni mashabiki wa kipato cha kawaida.

“Kuna mechi ambazo zina utamaduni wa kuvuta mashabiki wengi, kwa mfano unapocheza dhidi ya Simba au Yanga. Hizo ni timu kubwa, zina mashabiki lukuki na mara nyingi viingilio huwa vya juu zaidi jambo linalopunguza idadi ya watu,” amesema Chukuchuku.

Amesema kuna wakati wanapunguza viingilio ili kuendana na mazingira halisi ya uwanja, hasa kwenye mechi ambazo kihistoria hazivuti mashabiki wengi.

Pamoja na changamoto hizo, KMC inasema inaliona suala la idadi ndogo ya mashabiki kama changamoto inayoweza kutatuliwa kupitia mikakati ya makusudi ya ushawishi na uhamasishaji.

Amesema ofisi yake kwa sasa inaandaa mikakati ya mawasiliano na kampeni za ushiriki ambazo zitawaleta mashabiki karibu zaidi na timu, ikiwemo kufanya kazi na wadau wa mpira, mitandao ya kijamii na programu za kijamii Kinondoni.

“Tumepokea ushauri, tumepitia malalamiko na tumekuwa tukisikiliza mashabiki, lengo letu ni kufanya mechi za KMC ziwe sehemu ya burudani ya wakazi wa Kinondoni. Hivyo tunaweka mpango wa kuhakikisha kila mechi ya nyumbani inavutia mashabiki zaidi,” amesema Chukuchuku.

Amesema kwa sasa, uongozi wa KMC umeeleza kuwa uko katika hatua ya mwisho ya kukamilisha mkakati wao wa uhamasishaji, ambao utatangazwa hivi karibuni.

Athari za kushuka kwa mashabiki

Wachumi wanasema kupungua kwa mashabiki viwanjani si suala la hisia pekee, bali lina athari za moja kwa moja kwenye uchumi wa klabu zinazotegemea mapato ya siku ya mechi, tofauti na klabu zinavyopata nguvu kubwa kutoka kwa wadhamini.

Godfrey Nyasoti amesema, klabu nyingi bado zinategemea kwa kiasi kikubwa mapato ya viingilio kama chanzo kikuu cha fedha, hasa kwa mechi za nyumbani.

“Klabu zinaangalia kila shilingi ya kiingilio ni muhimu uwanja unapokosa watu, klabu inapoteza mapato ya tiketi, mauzo ya bidhaa na hata mvuto kwa wafanyabiashara wadogo waliopo kandokando ya uwanja,” amesema Nyasoti.

Amesema tofauti hiyo inaonekana wazi kwa klabu kubwa ambazo zina mikataba minono ya udhamini na haki za matangazo.

“Simba na Yanga, hata kama uwanja haujajaa, bado wana mapato ya uhakika kutoka kwa wadhamini wakuu, mauzo ya jezi na mikataba ya matangazo. Lakini klabu ndogo, mashabiki wakipungua, mapato yanaporomoka moja kwa moja,” amesema.

Kwa mujibu wa mchumi mwingine, Sophia Mussa, kushuka kwa mashabiki viwanjani pia kunapunguza thamani ya soka kama bidhaa ya burudani ya moja kwa moja, jambo linaloweza kuwaathiri hata wadhamini kwa muda mrefu.

“Mfanyabiashara anayetaka kudhamini klabu anaangalia uwanja umejaa kiasi gani, kelele za mashabiki na taswira ya tukio. Uwanja ukiwa mtupu, hata udhamini unakuwa hauna mvuto mkubwa,” amesema Sophia.

Amesema Dar es Salaam, ambako gharama za maisha na usafiri zimepanda, mashabiki wengi wanachagua TV kama mbadala wa bei nafuu.

“Kiuchumi, shabiki anauliza nauli, kiingilio, chakula na muda dhidi ya kutazama bure au kwa gharama ndogo nyumbani. Kwa wengi, hesabu haikai sawa hivyo anachagua sehemu ambayo hatotumia sana,” amesema.

Wachumi hao wanashauri klabu kuacha kutegemea viingilio pekee na kuwekeza zaidi kwenye mifumo mbadala ya mapato, ikiwemo bidhaa rasmi, programu za uanachama, matangazo ya kidijitali na uzoefu wa kipekee uwanjani.

Kwa mtazamo wao, kama hali ya kushuka kwa mashabiki itaendelea, klabu zinazotegemea zaidi viingilio zitaingia kwenye hatari ya kifedha, huku klabu zenye wadhamini zikibaki imara zaidi, jambo linaloweza kuongeza pengo la ushindani ndani ya Ligi Kuu Bara.

Bodi wanasemaje?

Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Karim Boimanda, amesema chanzo kikuu cha kupungua kwa mashabiki wanaojitokeza viwanjani, licha ya idadi ya wanaofuatilia Ligi Kuu kupitia runinga na mitandao ya kijamii kuongezeka kwa kasi ni kile alichokitaja kuwa ukosefu wa thamani ya burudani uwanjani, jambo linalowafanya mashabiki wengi kuamua kubaki nyumbani.

“Ukiangalia mashabiki wanaofuatilia ligi kupitia TV wanaongezeka, lakini idadi ya wanaokuja viwanjani inapungua. Tulijiuliza kwa nini? Jibu tukalipata thamani ya uwanjani haimshawishi shabiki kuja,” amesema Boimanda.

Amesema kwa muda mrefu mechi zimekuwa hazitoi burudani zaidi ya dakika 90 za mchezo, hali inayowafanya mashabiki kuhisi hawapati kitu cha ziada mbali na kutazama tu mpira.

“Shabiki anaingia uwanjani saa sita mchana, mechi inaanza saa kumi, kwa saa zote hizo anapata nini? Wengi wanajikuta wanaangalia nyasi tu. Hakuna burudani wala kitu kinachomfanya aone tofauti kati ya kukaa nyumbani na kuja uwanjani,” amesema.

Kutokana na changamoto hiyo, Bodi ya Ligi iliamua kufanya mabadiliko ya kanuni kwa kuweka sharti jipya kila uwanja lazima uwe na burudani ya muziki kabla ya mechi kuanza.

“Tukaweka kwenye kanuni kwamba lazima kuwe na burudani ya muziki, wasanii au chochote kinachowapa mashabiki raha kabla ya mchezo. Tukaona hilo ndio linaongeza thamani ya tukio zima la mechi,” amesema Boimanda.

Amesema mwanzoni jukumu hilo lilikuwa la Bodi ya Ligi, lakini baada ya marekebisho, mamlaka na wajibu mkubwa umepelekwa kwa klabu.

“Sasa hivi tumerudisha majukumu kwa klabu zenyewe ndizo zinapaswa kuhakikisha viwanja vina burudani na mashabiki wanapata jambo bora ndiyo maana klabu zimeanza kufanyia kazi zaidi kwa sababu zinajua ni wajibu wao,” amesema.

Boimanda amesisitiza kuwa kazi ya Bodi si kuongeza mashabiki viwanjani moja kwa moja, bali kuikuza thamani ya ligi ili klabu ziwe na urahisi wa kuwashawishi mashabiki wao.

“Bodi ya Ligi haina mashabiki, hivyo mashabiki ni wa klabu jukumu letu ni kuongeza thamani ya ligi, kuitangaza, kuifanya kuwa kubwa na yenye mvuto,” amesema.

Amesema thamani ya ligi imeongezeka kwa kiasi kikubwa na hilo limeifanya kuwa rahisi kutazamika ndani na nje ya nchi. “Sisi tumeshafanya kazi yetu tumeikuza ligi, tumeipa thamani, tumeitangaza. Sasa jukumu la kuongeza mashabiki uwanjani ni la klabu, wao ndio wauzaji wa tiketi,” amesema Boimanda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *