Dar es Salaam. Ubora anaouonyesha hadi sasa ndani ya JKT Tanzania ni dhahiri kabisa Salehe Karabaka ameyaanza maisha mapya ndani ya Klabu hiyo ambayo anaichezea kwa mkopo kutokea kwa Wekundu wa Msimbazi, Simba.
Kiungo huyo mshambuliaji alijiunga na Simba msimu wa 2023/2024 akitokea JKU ya Zanzibar, lakini hakupata nafasi ya kutosha kuitumikia Msimbazi, jambo ambalo lilimfanya akalie mbao ndefu.
Baada ya kukosa nafasi ya kutosha ndani ya Wekundu wa Msimbazi, Karabaka alipelekwa kwa mkopo kuitumikia Klabu ya Namungo msimu wa 2024/2025 na baada ya msimu huo kumalizika kiungo huyo alikuwa amepachika mabao mawili.
Hadi sasa akiwa anaendelea kuitumikia JKT Tanzania, kiungo huyo ameonyesha ubora wa hali ya juu akiwa amehusika katika mabao nane, akifunga sita na kutoa pasi mbili za mabao tangu ajiunge na Maafande hao msimu huu huku akiwa ndiye kinara anayeongoza mbio za ufungaji bora wa Ligi Kuu ya NBC.
Katika kikosi cha JKT Tanzania sasa hivi, Karabaka ametengeneza utatu sumbufu unaowajumuisha pia Paul Peter na Edward Songo.
Huyu Paul Peter naye amefunga mabao matatu akifuata katika orodha ya wafumania nyavu akiwa sambamba na Peter Lwasa wa Pamba Jiji, huku Songo yeye amepachika bao moja tu.
Ndani ya JKT Tanzania, Karabaka anatimiza kwa ufasaha kile ambacho kinapaswa kufanywa na mchezaji wa mkopo. Anacheza kwa kujituma na anaonyesha shauku ya kutaka kuisaidia zaidi timu hiyo.
Anaonyesha anafahamu kwamba Simba inapomtoa kwa mkopo haimuonei bali inataka apate nafasi kubwa ya kucheza na kuimarisha kiwango chake, ili pale itakapomrudisha aweze kuhimili ushindani wa nafasi katika kikosi chao.
Karabaka mwenye umri wa miaka 25, anatoa somo kwa wachezaji wenzake kwamba wanapotolewa kwa mkopo, ni fursa kwao kujiboresha zaidi na sio adhabu.
Mshambuliaji wa Simba, Salehe Karabaka (Wakwanza mbele kushoto) ambaye kwa sasa anakipiga kwa mkopo JKT Tanzania. Picha na Mtandao
KILICHOMNG’OA SIMBA
Karabaka aliwahi kuweka wazi kuwa kuondoka kwake Simba kulichochewa na ushindani mkali wa nafasi. Alisema aliamua kuomba kuondoka kwa mkopo ili kupata timu ambayo itampa nafasi ya kucheza mara kwa mara, jambo ambalo sasa analipata akiwa na JKT Tanzania.
“Nilifanya uamuzi huo kutokana na uwepo wa wachezaji waliokuwa wananinyima nafasi ya kucheza. Kocha aliwapa nafasi zaidi kutokana na uwezo wao,” alisema Karabaka.
Aliwataja Ellie Mpanzu, Kibu Denis, Ladack Chasambi na Joshua Mutale kuwa ni wachezaji waliokuwa wakimzidi na kumfanya aombe kuondoka.
Kwa mujibu wake, wachezaji hao wote ni bora na wenye uwezo mkubwa, na kocha ndiye aliyekuwa na maamuzi ya nani acheze na nani akae nje. Karabaka alikiri hakuwa na nguvu ya kumshawishi kocha ampe nafasi badala ya wengine.
Mshambuliaji wa Simba, Salehe Karabaka ambaye kwa sasa anakipiga kwa mkopo, JKT Tanzania. Picha na Mtandao
UJUMBE WA MZAMIRU
Si kila mchezaji anashtushwa na kutokuwepo kwa mchezaji fulani kambini, lakini Karabaka anamtaja Mzamiru Yassin kuwa baada ya kutomuona siku mbili tu mazoezini alinyanyua simu yake kumpigia.
“Sikuaga mtu zaidi ya kocha, meneja na viongozi. Wachezaji walikuwa hawafahamu ila Mzamiru ndio alikuwa mtu wa kwanza kunipigia kuniuliza niko wapi kutokana na kutoniona mazoezini,” alisema Karabaka na kuongeza:
“Simu yake ilikuwa njema sana kwangu kwani nilijihisi ni mtu mwenye bahati licha ya kukosa nafasi, lakini kuna watu walikuwa wanaona umuhimu wangu kuonekana ndani ya Simba. Nilifurahi sana na nikamwambia nimechagua kutoka kujaribu maisha mengine nje ya Simba.”
Karabaka alisema Mzamiru alimtakia kila la heri na kumwambia yeye ni mchezaji mzuri ana uwezo wa kufanya mambo makubwa ndani ya JKT Tanzania na ni timu sahihi kwake huku akimsihi apambane.
Kiungo huyo aliwahi kusema kuwa anayatamani maisha anayoyaishi sasa kwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara, akimshukuru kocha Ahmad Ally kumuamini na akimpa nafasi ya kucheza.
“Nawashukuru benchi la ufundi, wachezaji wenzangu kwa ushirikiano mzuri wanaonipa, pia mashabiki zangu ambao naahidi nitaendelea kufanya vizuri kila nitakapopata nafasi, kwani kuaminiwa kunanipa nguvu ya kuonyesha nilionao.
“Nitaendelea kuipambania JKT Tanzania iweze kufikia malengo tuliyojiwekea mwanzo wa msimu ikiwa ni pamoja na kumaliza nafasi tano za juu, na kwa sasa tunaongoza ligi ni sehemu nzuri kwetu, tutaendelea kupambana ili tusishuke,” alisema Karabaka.
Mshambuliaji wa Simba, Salehe Karabaka ambaye kwa sasa anakipiga kwa mkopo, JKT Tanzania. Picha na Mtandao
ANAVYOMKUBALI CHAMA
Kabla ya kujiunga Simba alikuwa anatamani siku moja acheze na mastaa kama kiungo Clatous Chama, Shomari Kapombe, Mzamiru Yassin na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye kwa sasa amejiunga na Yanga.
“Kabla ya Chama kuondoka kwenda Yanga nilimfuata na kumueleza jinsi ambavyo nilikuwa namkubali, alicheka na kuniambia dogo ndiyo mpira, akanipa ushauri wa kufanya mazoezi kwa bidii, nidhamu, kutochanganya ustaa na kazi ya uwanjani na alisema nina kipaji kikubwa, kisha nikapiga naye picha ya ukumbusho.
“Kapombe, Tshabalala na Mzamiru pia wananiambia nisikate tamaa, ikitokea nikipewa nafasi nionyeshe, ndiyo itakuwa mwanzo wa safari yangu ya kuaminiwa.”
Mshambuliaji wa Simba, Salehe Karabaka (Kulia) ambaye kwa sasa anakipiga kwa mkopo, JKT Tanzania., kushoto ni kipa wa zamani timu hiyo, Yakoub Suleiman, ambaye kwa sasa anakipiga Simba. Picha na Mtandao
FAIDA ZA KUWA STAA
Alipokuwa Simba, Karabaka aliwahi kusema kuna huduma za kijamii anazozipata kwa urahisi;
“Ikitokea nimepata tatizo basi napata msaada kwa haraka, ila changamoto inapotokea ukafanya vitu vya ovyo utaonekana kituko mbele za watu pia unakuwa unaichafua brandi ya klabu.”
Alimtaja kipa Hussein Abel alimsaidia kujua ukubwa wa klabu, kipi akifanye na mambo ya kuyaepuka.
“Simba ni tofauti na timu nilizocheza nyuma, nikagundua natakiwa kuzidisha nidhamu ya mazoezi na kuutumia muda wangu vizuri,” alisema.
Kuhusu dili lake lilikuaje hadi akajiunga Simba, alisema meneja wake Ally Mbasha ndiye aliyesimamia kila kitu na hakuwahi kuwaona watu ambao walizungumza na msimamizi wake huyo.
“Nilifurahi sana kupata fursa ya kucheza Simba, nakumbuka mechi ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya timu yangu ya zamani JKU nilifunga bao hivyo ni mchezo ambao umesalia katika kumbukumbu zangu,” alisema Karabaka ambaye pesa yake kubwa ya kwanza kuishika katika soka ilikuwa Sh80,000 mshahara aliokuwa anapokea mwisho wa mwenzi JKU.
Mshambuliaji wa Simba, Salehe Karabaka ambaye kwa sasa anakipiga kwa mkopo, JKT Tanzania. Picha na Mtandao
TUKIO ASILOLISAHAU
Haukumbuki mwaka isipokuwa tukio ambalo halijawahi kufutika katika maisha yake, walitoka timu za mtaani kufanya mazoezi, kocha akawapa nauli na rafiki yake Omary Mwapopo aliyekuwa beki wa kati, hakupanda daladala akaomba lifti ya bodaboda akapata nayo ajali na kufariki dunia.
“Baada ya dakika 10 akapata ajali akafariki dunia ila dereva bodaboda alipona, maana waliingia barabara kubwa wakagongwa na gari, sikuamini baada ya kusikia hadi nilipomkuta hospitali.
Ilinifunza kuona kifo hakina taarifa, maana dakika 10 kibinadamu ni chache ila kwa Mwenyenzi Mungu lolote linaweza likatokea, tulipanga mipango mingi ya soka pamoja, tuliamini siku moja tutakuwa na majina makubwa, lakini Mungu ndiye anajua siku zetu.”
Mshambuliaji wa Simba, Salehe Karabaka ambaye kwa sasa anakipiga kwa mkopo, JKT Tanzania. Picha na Mtandao
MAANA YA KARABAKA
Kuhusu jina la Karabaka, kiungo huyo alisema; “Sifahamu maana yake ingawa najua lina maana yake, nataka nifuatilie ili nijue.
“Ni mzaliwa wa Tanga kuna mila na desturi zetu, hilo jina nilipewa lilikuwa la ndugu yangu na niliwahi kuambiwa lina maana, lakini kwa kipindi hicho sikuzingatia hata kidogo, ila kwa sasa nahitaji kufahamu kama linaendana na maisha yangu,” alisema Karabaka anayempenda Vinicius jr mchezaji wa Real Madrid jinsi anavyotumia utulivu na akili kucheza mpira.