Dar es Salaam. Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves ameendelea kutamba katika Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya leo Jumatatu, Februari 9, kutangazwa kuwa Kocha Bora wa Ligi Kuu mwezi Januari.

Tuzo hiyo ni ya pili mfululizo kwa Pedro kwani ndiye aliibuka mshindi kwa tuzo za mwezi Desemba.

Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, imeeleza kuwa Pedro ameshinda tuzo hiyo akiwapiku Yusuph Chipo wa Mtibwa Sugar na Juma Mgunda wa Namungo FC.

Katika mwezi huo Januari, Pedro aliiongoza Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Dodoma Jiji na ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Mashujaa FC.

Wakati Pedro akishinda upande wa Kocha Bora, nyota wa Dodoma Jiji FC, Edgar William ameibuka mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora wa Januari.

William aliyeisaidia timu yake kupata ushindi katika michezo minne iliyocheza mwezi huo akifunga mabao matatu, amewashinda Aurelio Laurindo ‘Depu’ wa Yanga na Fabrice Ngoy wa Namungo FC.

Meneja wa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, Hussein Muhondo wa yeye ameibuka mshindi wa tuzo ya Meneja Bora wa Uwanja.

Katika Ligi ya Championship, Kocha Bora wa Januari ni Zuberi Katwila wa Geita Gold akiibuka mshindi kwa mara ya pili mfululizo.

Mchezaji wa Mbeya Kwanza, Joseph Ambukege ametangazwa mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora Januari wa Ligi ya Championship.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *