Tanga. Katibu Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF), Pradeep Kurukulasuriya ameungana na viongozi wa mkoa, wilaya na wananchi wa Kijiji cha Boma Subutini, Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, kuweka jiwe la msingi la kiwanda cha kisasa cha uchakataji mwani.

Kiwanda hicho kinajengwa kwa lengo la kuongeza ustahimilivu wa tabianchi, kuimarisha fursa za kiuchumi na kuboresha maisha ya watu wanaoishi maeneo ya pwani ya bahari.

Inaelezwa kuwa uwekaji wa jiwe la msingi unaashiria kuanza kwa ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo mashine za kuongeza thamani ya mwani na mifumo ya kukausha inayotumia nishati ya jua pamoja na utoaji wa mafunzo kwa wakulima kuhusu uchakataji, ufungashaji, udhibiti wa ubora na upatikanaji wa masoko.

Akizungumza leo Alhamisi Juni 25, 2026 katika hafla iliyofanyika kijijini hapo, Kurukulasuriya amesema ni muhimu fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kuwafikia moja kwa moja wananchi wanaoathirika zaidi na changamoto hizo.

“Leo hatuweki tu jiwe la msingi. Tunaweka msingi wa mustakabali wenye ustahimilivu zaidi, ustawi na maendeleo endelevu kwa wananchi wa Mkinga. Uwekezaji huu unaonyesha jinsi fedha za tabianchi zinavyoweza kuziwezesha jamii kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi huku zikichochea ajira, kuongeza kipato na kulinda rasilimali za asili,” amesema.

Amesema Wilaya ya Mkinga ni miongoni mwa maeneo yanayoathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi mkoani Tanga kutokana na ukame wa mara kwa mara, mabadiliko yasiyotabirika ya mvua, uharibifu wa mifumo ikolojia, kuongezeka kwa kina cha bahari na kupungua kwa fursa za kiuchumi.

Kwa mujibu wa Kurukulasuriya, kupitia Mpango wa LoCAL, miradi ya kukabiliana na athari za tabianchi itatekelezwa katika vijiji 11 vya wilaya hiyo.

Amesema mradi wa uchakataji mwani ni sehemu ya programu pana ya ustahimilivu wa tabianchi yenye thamani ya takribani Sh739 milioni, inayotarajiwa kunufaisha wananchi 17,494 katika vijiji 11 vya Wilaya ya Mkinga.

Programu hiyo inajumuisha uwekezaji katika miradi ya umwagiliaji inayozingatia mabadiliko ya tabianchi, miundombinu ya maji kwa mifugo, ufugaji wa nyuki wa kisasa, uongezaji thamani wa asali, matumizi ya nishati safi ya kupikia mashuleni, uhifadhi wa mifumo ikolojia pamoja na usimamizi endelevu wa rasilimali za asili.

Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Gilbert Kalima amesema ushirikiano unaoendelea kati ya UNCDF, washirika wa maendeleo na Serikali ya Tanzania unalenga kusaidia utekelezaji wa miradi ya kukabiliana na athari za tabianchi inayotokana na mahitaji halisi ya wananchi.

Kwa upande wao, wakulima wa mwani na viongozi wa umma wamesema kiwanda hicho kitasaidia kuboresha uchakataji wa mazao yao ya mwani, kuongeza ubora sambamba na kuimarisha ushindani wa soko na kuongeza kipato cha kaya zinazotegemea zao hilo.

Mpango wa LoCAL ni mfumo wa kimataifa unaowezesha fedha za tabianchi kuelekezwa moja kwa moja kwa mamlaka za serikali za mitaa kupitia mfumo wa ruzuku zinazozingatia matokeo katika kujenga ustahimilivu wa tabianchi.

Kupitia mfumo huo, serikali za mitaa huwezeshwa kutambua, kupanga, kutekeleza, kufuatilia na kuripoti uwekezaji wa miradi ya ustahimilivu wa tabianchi ndani ya mifumo rasmi ya Serikali.

Nchini Tanzania, mpango huo unalenga kuimarisha uwezo wa mamlaka za serikali za mitaa katika kujenga ustahimilivu wa jamii dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi huku ukichochea maendeleo ya kiuchumi yanayozingatia mazingira.

Ujenzi wa kiwanda hicho unatarajiwa kuwa mfano wa namna ushirikiano kati ya Serikali, washirika wa maendeleo na jamii unavyoweza kuleta suluhisho endelevu kwa changamoto za tabianchi, huku ukiongeza fursa za kiuchumi na kuboresha ustawi wa wananchi wa maeneo ya pwani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *