
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema kuwa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Marekani na Iran yanatoa fursa nzuri ya kufikia suluhu “inayoridhisha pande zote ” kuhusu suala la nyuklia la Iran.
Rais Pezeshkian ametoa kauli hiyo wakati wa hafla ya kuadhimisha miaka 47 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu jijini Tehran, hafla iliyohudhuriwa na mabalozi wa nchi za kigeni.
Amesema:“Duru mpya ya mazungumzo ya nyuklia, ambayo imeanza nchini Oman kwa msaada na ushirikiano wa majirani zetu, ni fursa nzuri ya kupata suluhu ya haki, ya kimantiki, ya usawa na inayokubalika kwa pande zote.”
Rais amebainisha kuwa Iran inataka dhamana ya haki yake ya kurutubisha madini ya urani chini ya Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT) pamoja na kuondolewa kwa vikwazo, huku akieleza matumaini kuwa upande wa pili utaachana na madai ya kupindukia ili kuruhusu kupatikana kwa matokeo yanayotarajiwa.
Amesema pia kwamba: “Ujumbe wetu kwa dunia uko wazi: Iran ni nchi inayotimiza ahadi zake, mradi tu ionyeshwe uaminifu na kuheshimiwa kwa makubaliano kutoka upande wa pili.”
Aidha, Rais Pezeshkian amesema kuwa mazungumzo ni njia endelevu ya kukabiliana na changamoto za kikanda na za kimataifa.
Rais wa Iran ameongeza kuwa sera ya nje ya Tehran inaongozwa na misingi ya mwingiliano wa heshima na hadhi.
Aidha amesema Iran inakaribisha mazungumzo yoyote yanayozingatia sheria za kimataifa, heshima, na kulinda mamlaka ya kitaifa, kwa msingi wa usawa wa pande zote na kwa kuzingatia kanuni ya ushindi wa pamoja.
Mazungumzo ya hivi karibuni yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani yalifanyika Muscat, Oman, tarehe 6 Februari, baada ya wiki kadhaa za kuongezeka kwa mvutano uliosababishwa na Marekani kuongeza vikosi vyake vya kijeshi katika eneo la Asia Magharibi pamoja na vitisho vyake vya kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, aliyeongoza ujumbe wa Tehran, alizitaja mazungumzo hayo kama “mwanzo mzuri,” akisema kuwa pande zote zimekusudia kuendelea na majadiliano.