Chanzo cha picha, Reuters
Wapalestina, nchi za Kiarabu, makundi ya Waisraeli yanayopinga uvamizi, pamoja na Uingereza, wamezikosoa vikali hatua mpya zilizoidhinishwa na baraza la usalama la Israel kuhusu Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu. Wanasema hatua hizo ni sawa na kudhibiti rasmi eneo hilo kwa vitendo.
Hatua hizo zilitangazwa na Waziri wa Hazina wa Israel mwenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia, Bezalel Smotrich. Alisema zitafanya iwe rahisi zaidi kwa walowezi wa Kiyahudi kuchukua ardhi ya Wapalestina. Aliongeza akisema: “Tutaendelea kuua wazo la taifa la Palestina.”
Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, makazi yote ya walowezi yanachukuliwa kuwa haramu.
Hatua hizo ambazo zinatarajiwa kuidhinishwa rasmi na kamanda mkuu wa kijeshi wa Israel anayesimamia Ukingo wa Magharibi, zinalenga kuongeza udhibiti wa Israel katika eneo hilo, hasa katika masuala ya umiliki wa ardhi, mipango ya ujenzi, utoaji wa vibali na utekelezaji wa sheria.
Wapalestina wamesema wana hofu kuwa mabadiliko hayo yataongeza shinikizo kwa watu binafsi kuuza ardhi yao, pamoja na kusababisha vitendo vya kughushi hatimiliki na udanganyifu.
Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas ambaye anaongoza Mamlaka ya Palestina (PA) inayosimamia sehemu za Ukingo wa Magharibi, alizitaja hatua hizo kuwa “hatari” na kuwa ni “jaribio la wazi la Israel kuhalalisha upanuzi wa makazi ya walowezi, kunyang’anya ardhi na kubomoa mali za Wapalestina, hata katika maeneo yaliyo chini ya mamlaka ya Palestina.”
Abbas amezitaka Marekani na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuingilia kati mara moja.
Kwa pamoja, mawaziri wa mambo ya nje wa Misri, Jordan, Umoja wa Falme za Kiarabu, Indonesia, Pakistan, Uturuki, Saudi Arabia na Qatar wamesema tangazo hilo “linaharakisha juhudi haramu za kuitwaa Ukingo wa Magharibi na kuwafukuza wananchi wa Palestina.”