DAR ES SALAAM: Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za magonjwa yasiyoambukiza makali kwa kusogeza huduma hizo karibu na wananchi, hususan katika hospitali za wilaya na vituo vya afya vilivyochaguliwa nchini.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa imewezesha wagonjwa wengi kupata huduma za uchunguzi, matibabu na ufuatiliaji wa magonjwa hayo bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kwenda hospitali za rufaa za mikoa au taifa.
Akifungua Mkutano Mkuu wa Tatu wa Kimataifa wa Kimkakati wa Kikanda wa PEN-Plus (ICPPA 2026) jijini Dar es Salaam leo Juni 23, 2026 kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesema mkakati wa PEN-Plus umeendelea kuwa suluhisho muhimu kwa nchi za Afrika katika kuboresha huduma za magonjwa yasiyoambukiza makali.

Alisema Serikali ya Tanzania imefanya mapitio ya Miongozo ya Matibabu ya Taifa pamoja na Orodha ya Dawa Muhimu ili kuwezesha utoaji wa huduma maalumu za kitabibu katika ngazi ya huduma za afya ya msingi.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, huduma hizo zinajumuisha tiba ya ndani, huduma za dharura, upasuaji wa kawaida, huduma za uzazi na magonjwa ya wanawake pamoja na huduma za watoto.
Aidha, amesema kupitia ushirikiano wa Serikali, washirika wa maendeleo na Mpango wa Samia Suluhu Hassan Outreach, huduma za PEN-Plus zinaendelea kupanuliwa nchini kote, hasa katika maeneo ya vijijini na yale yenye changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya.
Mchengerwa amesema upanuzi huo wa huduma unachangia kuimarisha usawa katika upatikanaji wa huduma za afya, kupunguza gharama za matibabu kwa wagonjwa na familia zao, pamoja na kupunguza vifo vya mapema vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza ambavyo vinaweza kuzuilika.

Mchengerwa amesema magonjwa hayo yanajumuisha kisukari, shinikizo la damu, saratani, magonjwa ya moyo na magonjwa mengine sugu ambayo yanaendelea kuathiri mamilioni ya watu duniani.
Amesema kwa upande wa Tanzania, takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa yasiyoambukiza husababisha zaidi ya vifo milioni 43 kila mwaka duniani, sawa na takriban asilimia 74 ya vifo vyote, huku watu wengi wakifariki kabla ya kufikisha umri wa miaka 70.
“Hali hii inaonesha ukubwa wa changamoto inayoukabili mfumo wa afya duniani na Afrika kwa ujumla. Afrika imeendelea kubeba mzigo mkubwa wa vifo vya mapema vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza, jambo linaloifanya changamoto hii kuwa si ya kiafya pekee bali pia ya kiuchumi na kijamii,” amesema.
Mchengerwa amesema vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza vimeongezeka kutoka chini ya asilimia 25 katika miaka ya 1980 hadi kufikia asilimia 39 mwaka 2021.
Amesema magonjwa ya moyo yameongezeka na kuathiri takriban asilimia 20 ya wananchi, huku saratani pekee ikisababisha karibu vifo 45,000 kila mwaka nchini.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, magonjwa hayo yameendelea kuongeza mzigo mkubwa wa kifedha kwa familia na serikali kutokana na gharama kubwa za matibabu, ambapo huduma za saratani na usafishaji damu (dialysis) zinachukua takriban asilimia 20 ya malipo yote ya bima ya afya kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Aidha, amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa mkakati wa PEN-Plus unaolenga kupeleka huduma za uchunguzi, matibabu na ufuatiliaji wa magonjwa yasiyoambukiza makali katika hospitali za wilaya na vituo vya afya ili kuwafikishia wananchi huduma karibu na maeneo wanayoishi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani kanda ya Afrika Prof. Mohamed Janabi amesema mkakati huo una umuhimu mkubwa katika kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza barani Afrika.
Amesema magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, figo na saratani yamekuwa changamoto kubwa ya kiafya barani Afrika, na hivyo yanahitaji mkakati madhubuti unaowalenga wananchi katika ngazi ya huduma za msingi.
“Mpango wa PEN-PLUS unalenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za kibingwa kwa kuzipeleka karibu zaidi na wananchi kupitia hospitali za wilaya na vituo vya afya, badala ya wagonjwa kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu katika hospitali kubwa za rufaa”, amesema Prof. Janabi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuongeza uwekezaji wa ndani katika sekta ya afya ili kupunguza utegemezi wa misaada ya nje, akieleza kuwa mzigo wa magonjwa yasiyoambukiza unaendelea kukua na unahitaji suluhisho endelevu linalotokana na rasilimali za ndani.
Prof. Janabi amesema iwapo mpango wa PEN-PLUS utatekelezwa kikamilifu, utakuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha huduma bora za afya kwa wote (Universal Health Coverage) na kupunguza kwa kiwango kikubwa vifo vinavyosababishwa na magonjwa yasiyoambukiza barani Afrika.