
Dakika chache baada ya kufunga bao lake la kwanza katika Kombe la Dunia Jumapili iliyopita, mchezaji wa timu ya taifa ya Uhispania, Lamine Yamal alijikuta akikabiliwa na wimbi kubwa la mashambulizi kwenye mitandao ya kijamii baada ya kusujudu akimshukuru Mungu kwa bao alilofunga dhidi ya timu ya taifa ya Saudi Arabia kwenye mashindano ya Kombe la Dunia FIFA 2026.
Suala hilo liliwakasirisha sana wanamitandao wa mrengo wa kulia wa Uhispania na Ulaya kwa ujumla, ambao hawakuliona kama jambo la kupita, bali wanalitaja kuwa ni “Kuisilimisha” timu ya taifa ya soka ya Uhispania!
Hujuma dhidi ya Lamine Yamal baada ya kusujudu akimshukuru Mungu kwa kufunga bao lake la kwanza katika mashindano ya Kombe la Dunia haikujikita katika kukosoa jinsi kitendo hicho kilivyofanyika, bali imehoji uhusiano wa Yamal na timu ya taifa ya Uhispania, na kutumia asili yake ya Morocco na utambulisho wake wa kidini katika hujuma ya wazi ya kibaguzi inayomlenga nyota huyo wa soka kama mmoja wa wahamiaji na Waislamu.
Ufuatiliaji wa jina la Lamine Yamal kwenye jukwaa la “X” unaonyesha kwamba mashambulizi dhidi yake hayakuanza baada ya kusujudu akisherehekea goli lake dhidi ya Saudia Arabia, bali yalianza saa chache kabla ya mechi hiyo, kufuatiia mjadala ulioibuliwa na makala iliyochapishwa na gazeti la Uingereza, The Telegraph, yenye kichwa cha maneno: “Lamine Yamal wa Sasa ni Tofauti Sana na Mvulana Ambaye Alionekana kwenye Euro.”
Makala hiyo ilijadili misimamo ya hivi karibuni ya Yamal, hasa msimamo wake wa kupinga ubaguzi wa rangi katika mechi ya kirafiki dhidi ya Misri mnamo Machi 31, na kupeperusha kwake bendera ya Palestina wakati wa sherehe za ubingwa wa timu ya Barcelona katika Ligi Kuu ya Uhispania.
Mwandishi wa The Telegraph alimshambulia Yamal akielezea vitendo hivyo kuwa “vinazusha utata,” akiongeza kwamba vinaonyesha hisia ya mchezaji kuhusu thamani na ushawishi wake na hamu yake ya kutumia sauti yake badala ya kukaa kimya.
Hujuma ya gazeti hilo la Uingereza imekabiliwa na ukosoaji mkubwa, huku akaunti nyingi zikisema kwamba makala hiyo inatambua mshikamano wa mwanasoka huyo na watu wa Palestina kama dhambi ya kisiasa. Mwanaharakati mmoja ameandika kwamba Lamine Yamal alitambuliwa kama “mtoto mwema” hadi alipopeperusha bendera ya Palestina, akiongeza kwamba waandishi wa habari ambao kihistoria waliwaandama wanariadha kama Muhammad Ali sasa wanawaadhibu wale wanaojaribu kutumia sauti zao kwenye kadhia zenye maana.
Makala hiyo ilisambaa zaidi baada ya Yamal kusujudu uwanjani, na ujumbe wa Twitter unaohusiana na kitendo hicho uliwafikia maelfu ya watu na kutazamwa na mamilioni ya watazamaji, kabla ya picha ya kitendo hicho kuwa cheche ya kampeni pana zaidi dhidi ya Yamal.
Wengi wamekosoa maelezo ya makala hiyo iliyotaja uungaji mkono wa mchezaji huyo kwa Palestina kuwa ni wenye utata, huku mwanablogu mmoja akisema: “Inatisha jinsi vyombo vya habari vinavyokushambulia mara tu unapoonyesha mshikamano na watu wa Palestina.”
Uchambuzi uliofanywa na the Open Source Unit unaonyesha kwamba shambulio lililofuata kusujudu kwa Yamal lilianzishwa na mitandao ya mrengo wa kulia ya Uhispania inayopinga Uislamu na Waislamu, na kusifu imani ya Kikristo.
Kama mfano tu, Akaunti ya “Canario Today”, ambayo inajihusisha na habari za wahamiaji, imetoa maoni ikisema “Uhispania ni nchi ya Kikristo, si ya Kiislamu,” katika chapisho lililotazamwa na maelfu ya watu ndani ya saa chache.