
Kuibuka kwa Mikunde
Mikunde, ikiwemo maharagwe ya kawaida, kunde na mbaazi, ni mbegu zinazoliwa za mimea ya familia ya legumes na zimekuwa zikiliwa kwa karne nyingi. “Mbegu hizi ndogo ni hazina ya lishe,” amesema Dr. Qu Dongyu Mkurugenzi Mkuu wa FAO, akisisitiza kwamba jamii ya mikunde ambayo ina vitamini, madini, na protini ni muhimu kwa lishe bora duniani.
Siku hii, iliyotangazwa rasmi na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, inatokana na mafanikio ya Mwaka wa Kimataifa wa Mikunde 2016.
FAO inatumia fursa hii kuhimiza jamii ya mikunde kama nyenzo ya kufanikisha Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu, ikikuza mifumo ya chakula inayojumuisha wote, yenye uthabiti, na inayohifadhi mazingira.
Nguzo ya mifumo endelevu ya chakula
FAO inasisitiza kwamba mikunde sio faida ya chakula tu bali pia husaidia mazingira. “Mikunde hubadilisha nitrojeni kutoka hewani hadi ardhini, kuimarisha bioanuwai, na kupunguza haja ya mbolea za kemikali,” amesema mtaalamu wa kilimo wa FAO. “Kujumuisha mikunde katika mifumo ya kilimo ni faida kwa wakulima na kwa mazingira.”
Shirika hilo pia linaonesha faida za kiuchumi na kijamii za uzalishaji wa mikunde. Mikunde huunda ajira kwa wanawake na vijana wa vijijini, kusaidia maisha yao huku wakisaidia uhakika wa chakula wa jamii.
Aina mbalimbali za mikunde
Mikunde inapatikana katika rangi nyingi na aina mbalimbali mfano nyekundu, kijani, nyeupe, nyeusi, na kahawia.
Uhai wa mikunde ni mrefu, ina wingi wa lishe, na uwezo wa kupunguza upotevu wa chakula unafanya kuwa viambato vinavyofaa kwa lishe endelevu. “Kutoka jikoni hadi shambani, mikunde ni muhimu katika kujenga jamii zenye afya na uthabiti,” limesema shirika la FAO ilisema.
Wito wa kimataifa
FAO inahimiza serikali, sekta binafsi, mashirika wadau, na umma kuongeza uzalishaji na matumizi ya mikunde.
“Siku ya Mikunde Duniani si sherehe tu ni wito wa kuchukua hatua kwa ajili ya mazingira bora, lishe bora, na maisha bora kwa wote,” imesema FAO.
Kuangaliamustakbaliwa Mikunde
Kadiri mikunde inavyoendelea kutambuliwa kwa jukumu lake katika kilimo endelevu na lishe, FAO inahimiza watumiaji duniani kote kujumuisha mbegu hizi katika lishe zao.
“Kila mkunde ni muhimu,” shirika hilo liliweka bayana. “Ni mbegu ndogo, lakini athari yake ni kubwa kwa watu, jamii, na sayari.”