
Dodoma. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amewataka Watanzania kujenga utamaduni wa kurudisha fadhila katika taasisi za elimu walizosomea kwa kusaidia kuboresha miundombinu ya shule na vyuo mbalimbali nchini.
Kichere ametoa wito huo leo Jumamosi, Juni 27, 2026, wakati akizungumza na wanafunzi na wahitimu wa zamani wa Chuo cha Shinyanga Commercial Institute (Shycom), ambao wanapanga kuandaa mbio za hisani kwa lengo la kuchangisha fedha za kuboresha miundombinu ya chuo hicho.
Amesema ni muhimu kwa watu waliopitia katika taasisi mbalimbali za elimu kurudisha mchango wao kwa maendeleo ya maeneo hayo, ili kusaidia kizazi cha sasa na kijacho kupata mazingira bora ya kujifunzia.
“Lazima tujenge utamaduni wa kurudisha shukrani katika maeneo ambayo tulipita na tukapata mafanikio. Nawaomba Wana Shycom tujitokeze kwa wingi katika mbio hizi ili tufanikishe malengo yetu,” amesema Kichere.
Kwa upande wake, Balozi Dk Pindi Chana akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amesema mpango huo unalenga kukusanya fedha kwa ajili ya maboresho ya zahanati ya chuo, ununuzi wa vitanda vya bweni la wavulana pamoja na kuboresha njia za miguu kutoka mabwenini.
Dk Chana ambaye pia ni miongoni mwa wahitimu wa chuo hicho, amesema huu ni mwendelezo wa jitihada za awali zilizofanyika mwaka 2024 ambazo zilifanikiwa kuchangisha takribani Sh200 milioni zilizotumika kuboresha mabweni ya wanafunzi.
“Nawahamasisha wote tuliosoma Shycom tuungane katika msafara huu wa Mapendo Sports ili tukaijaze Shinyanga. Twendeni tukaisaidie Serikali katika chuo chetu, tukumbuke kuwa kutoa ni moyo,” amesema Dk Chana.
Ameongeza kuwa wahitimu wanapaswa kujisajili na kutumia muda huu kuwatafuta wenzao waliopo ndani na nje ya nchi ili kufanikisha mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Septemba 26, 2026, ambazo zinaelezwa kuwa na lengo la kuwa za kihistoria kwa mji wa Shinyanga.
Naye Mkuu wa Chuo hicho, Dk John Nandi amesema michango iliyotolewa na wahitimu hao katika awamu ya kwanza mwaka 2024, ilisaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto za miundombinu zilizokuwa zikikikabili chuo hicho.
Amesema ushirikiano huo unaendelea kuacha alama muhimu si tu kwa chuo bali pia kwa jamii na taifa kwa ujumla, huku akiwahimiza wahitimu kutokata tamaa katika kuendelea kuchangia maendeleo ya taasisi hiyo.
“Mchango wenu unaweka alama kwa vizazi vya sasa na vijavyo, na ni kwa faida ya taifa letu pia,” amesema Dk Nandi.