Wakati mapigano makali yakiendelea kati ya washirika wa zamani wa  Jeshi la Sudan SAF na vikosi vya Msaada wa Haraka RSF pamoja na washirika wao Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, limesema kuwa katika baadhi ya maeneo ya jimbo la Darfur Kaskazini  zaidi ya nusu ya watoto wote wanakabiliwa na utapiamlo mkali.

Onyo hilo limefuatia kuchapishwa kwa takwimu mpya kutoka mfumo wa tathimini ya uhakika wa chakula IPC, unaofuatilia uhakika wa chakula duniani kwa msaada wa Umoja wa Mataifa, kutoka maeneo matatu Um Baru, Kernoi na At Tine ambayo yanaonesha viwango vya “janga kubwa vya utapiamlo.”

Njaa kali na utapiamlo huwakumba watoto kwanza wachanga, wadogo na walio hatarini zaidi, amesema msemaji wa UNICEF, Ricardo Pires.

Nchini Sudan, hali hii inaenea. Hawa ni watoto wenye umri kati ya miezi sita hadi miaka mitano, na muda wao unaisha.

Njaa inasambaa

UNICEF imesisitiza kuwa vizingiti vya kutangaza baa la njaa vimevukwa katika maeneo ambayo awali hayakuchukuliwa kuwa hatarini, kama vile Um Baru na Kernoi.

Migogoro, ufurushwaji mkubwa wa watu, kusambaratika kwa huduma za msingi na kuzuiwa kwa upatikanaji wa misaada hali zilizosababisha tahadhari za njaa katika maeneo hayo zinapatikana “katika maeneo makubwa ya Sudan,” amesisitiza Pires.

“Ikiwa baa la njaa linaonekana huko, linaweza kushika kasi popote,” ameonya.

Pires pia ameonya kuhusu kuenea kwa magonjwa kama tishio jingine kubwa kwa maisha ya watoto:

“Watoto hawa hawana njaa tu, karibu nusu ya watoto wote katika At Tine walikuwa wagonjwa ndani ya wiki mbili zilizopita. Homa, kuharisha, maambukizi ya njia ya hewa, kiwango cha chini cha chanjo, maji yasiyo salama na mfumo wa afya unaoporomoka vinageuza magonjwa yanayotibika kuwa hukumu ya kifo kwa watoto ambao tayari wanakabiliwa na utapiamlo.”

Ameutaka ulimwengu “kuacha kupuuza mateso ya watoto wa Sudan, akionya kuwa zaidi ya nusu ya watoto katika eneo la Um Baru, Darfur Kaskazini, wanaendelea kudhoofika huku tukitazama.”

Msemaji huyo wa UNICEF ameongeza kuwa “Hizi si takwimu tu. Hawa ni watoto wenye majina na mustakabali unaoporwa,”.

Takriban miaka mitatu tangu vita vilipozuka kati ya Jeshi la Sudan na RSF, watu milioni 13.6 wamelazimika kuyahama makazi yao, wakiwemo milioni 9.1 waliokimbia ndani ya nchi.

Huduma za afya zashambuliwa

Mwakilishi wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO, nchini Sudan, Dkt. Shible Sahbani, amewaambia waandishi wa habari kuwa licha ya wakimbizi kuhitaji huduma za afya kwa dharura, mfumo wa afya “umeharibiwa vibaya kutokana na mashambulizi, upotevu na uharibifu wa vifaa na dawa, upungufu wa wahudumu wa afya na ukosefu wa fedha za uendeshaji.”

Tangu vita vilipoanza Aprili 2023, WHO imethibitisha mashambulizi 205 dhidi ya huduma za afya, yaliyosababisha vifo 1,924 na majeruhi 529, amesema Dkt. Sahbani.

“Mashambulizi kama haya huinyima jamii huduma za afya kwa miaka mingi, huwatia hofu wagonjwa na wahudumu wa afya, na kuunda vikwazo vikubwa dhidi ya matibabu ya kuokoa maisha,” ameongeza.

Wakati huo huo, Sudan inakabiliwa na milipuko mingi ya magonjwa, yakiwemo kipindupindu, malaria, dengue na surua.

Ingawa WHO na washirika wake wanaendelea kusaidia kudhibiti milipuko hiyo, Dkt. Sahbani amesisitiza umuhimu wa ufikiaji mkubwa zaidi na ulinzi wa wahudumu wa afya na vituo vyao, kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu.

Wagonjwa na wahudumu wa afya hawapaswi kuhatarisha maisha yao wanapotafuta au kutoa huduma, amesema akiongeza kwamba “Zaidi ya yote, tunatoa wito wa amani. Sudan imesubiri amani kwa muda mrefu sana.”

Wito huo umeunga mkono kauli ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Türk, ambaye Jumatatu alitoa tena tahadhari kuhusu mgogoro mbaya nchini Sudan, alipolihutubia Baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva kuhusu “janga la haki za binadamu ambalo lingeweza kuzuilika” lililotokea katika mji wa El Fasher, Darfur Kaskazini, Oktoba mwaka jana.

Maelfu ya watu waliuawa huko ndani ya siku chache baada ya mzingiro wa miezi 18 wa mji hio, kulingana na ushuhuda uliokusanywa na ofisi ya Türk.

Hatari ya kuenea hadi Kordofan

Amesema hatari mpya ni uwezekano wa kurudiwa kwa ukiukaji huo katika eneo la Kordofan.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari mjini Geneva kuhusu ushiriki wa nchi nyingine katika mgogoro huo, msemaji wa Kamishna Mkuu, Ravina Shamdasani, amesisitiza wasiwasi wake kuhusu iwapo mataifa mengine yanahusika moja kwa moja, kuwepo kwa mamluki kutoka nchi mbalimbali, au iwapo yanatoa silaha, taarifa za kijasusi, ufadhili au msaada mwingine, au kushiriki katika uchumi wa kisiasa wa mgogoro wa Sudan.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *