
Taarifa hiyo imetolewa jijini Geneva, nchini Uswisi, ikieleza kuwa mapigano mapya kati ya jeshi la serikali kuu ya Ethiopia na vikosi vya serikali ya eneo la Tigray yameanza tangu tarehe 26 Januari, hasa katika maeneo ya Tselemti na Laelay Tselemti. Hali hii inasababisha hofu kubwa ya kurejea kwa uvunjifu wa haki za binadamu katika ukanda huo ambao bado una makovu ya vita vya miaka iliyopita.
Türk ameeleza kusikitishwa kwake na matumizi ya silaha nzito zikiwemo ndege zisizo na rubani na mizinga ambazo zimekuwa zikitumiwa na pande zote mbili, jambo linalowaweka raia kwenye hatari kubwa. Hivyo amesisitiza umuhimu wa mazungumzo akisema, “lazima kuwepo na juhudi za pamoja na endelevu kutoka kwa pande zote, kwa msaada wa jumuiya ya kimataifa, ili kupunguza mivutano kabla ya kuchelewa. Mazungumzo ya kisiasa na hatua za kujenga imani zinahitajika kwa haraka, sio kurejea tena kwenye ghasia za silaha.
Raia wanataabika kutokana na mapigano
Hali ya usalama imezidi kuwa tete huku kukiwa na ripoti za watu kukamatwa na kufungwa na pande zote mbili kwa tuhuma za kuegemea upande wa adui, jambo ambalo limekuwa likiendelea hata baada ya vikosi vya Tigray kujiondoa kwenye maeneo ya kaskazini-magharibi mwa jimbo hilo la Tigray. Türk amelaani vitendo hivyo akisema, “raia wapo njia panda, katikati ya mivutano inayoongezeka, huku kukiwa na ripoti kuwa pande zote mbili zinafanya ukamataji kwa sababu tu ya kuhisi watu wana mahusiano na upande mwingine. Jambo hili lazima likome.”
Zaidi ya raia milioni moja bado wamekimbia makazi yao tangu vita vya mwaka 2020-2022, na machafuko haya mapya yanatishia kuongeza idadi ya wakimbizi wa ndani. Türk amezitaka pande zote kurudi nyuma na kutatua tofauti zao kwa njia ya amani, huku akionya kuwa hata mivutano kati ya Ethiopia na nchi jirani ya Eritrea inaweza kufanya hali kuwa mbaya zaidi katika ukanda mzima hivyo ni lazima uchunguzi wa kina ufanyike kwa ukiukaji wowote wa haki za binadamu uliofanyika bila kujali ni nani amefanya.