Dar es Salaam. Benito Antonio Martínez Ocasio, ndilo jina halisi la Bad Bunny. Moja ya wasanii wenye ushawishi mkubwa katika muziki wa kizazi hiki.
Alizaliwa Machi 10, 1994, huko Bayamón, Puerto Rico na kukulia kijiji cha Vega Baja. Akilelewa katika familia ya tabaka la kati. Baba yake alikuwa dereva wa lori na mama yake mkufunzi wa Kiingereza.
Bad Bunny alipopokea tuzo ya Grammy 2026 ‘Albamu Bora ya Mwaka’
Bad Bunny alianza kuimba akiwa mdogo, akijifunza muziki kanisani kabla hata hajafikisha miaka 13. Alianza kuunda midundo yake mwenyewe na kuandika mistari ya muziki akiwa shuleni, huku akitumia muda wake wa ziada kujifunza zaidi kuhusu muziki.
Jina lake la sanaa ‘Bad Bunny’ lilitokana na picha yake ya utotoni akiwa amevaa koti la sungura. Picha ambayo ilamfanya aitumie kwenye kupata jina kwani aliamini kwenye biashara itakuwa rahisi watu kukumbuka kirahisi.
Alisomea katika Chuo Kikuu cha Puerto Rico, Arecibo. Lakini wakati huohuo alianza kupakia nyimbo zake kwenye SoundCloud mwaka 2013. Ilipofika mwaka 2016, wimbo wake ‘Diles’ ulimvutia mtayarishaji wa muziki maarufu DJ Luian na kumpa mkataba wake wa kwanza wa kurekodi, jambo lililomuwezesha kuingia rasmi kwenye tasnia ya muziki.
Bad Bunny aliwahi kufanya kazi katika duka la vyakula (supermarket) linaloitwa Econo huko Puerto Rico kabla hajapata umaarufu mkubwa kwenye muziki. Wakati huo alikuwa bado anasoma katika chuo. Dukani hapo alikuwa akifanya kazi kama mpangaji na mfungaji wa bidhaa dukani hapo
Inasemekana wimbo wake ‘Diles’ ulipoanza kupata umaarufu mtandaoni , ndipo alipoacha kazi dukani na kuingia rasmi kwenye muziki.
Muziki wake ulipata mwamko mkubwa zaidi aliposhirikiana na wasanii maarufu kama Cardi B na J Balvin kwenye wimbo ‘I Like It’ (2018). Wimbo huo ukawa wa kwanza kwa Bad Bunny kushika nafasi ya kwanza kwenye Billboard Hot 100.
Alipoachia albamu yake ya kwanza ‘X 100PRE mwaka 2018, ilionyesha uwezo wake mkubwa kwa kuimba aina mbalimbali za muziki.
Bad Bunny kwenye Super Bowl Halftime
Tangu wakati huo, albamu zake kadhaa ziliendelea kufanikiwa, ikiwemo ‘Un Verano Sin Ti’, ‘Nadie Sabe Lo Que Va a Pasar Mañana’, na ‘Debí Tirar Más Fotos’ albamu ya mwaka ambayo ilishinda Tuzo ya ‘Album of the Year’ kwenye tuzo za Grammy kwa mara ya kwanza kwa albamu yote kwa lugha ya Kihispania mwaka 2026.
Bad Bunny akitumbuiza kwenye Super Bowl Halftime
Amejikuta akijizolea mashabiki wengi kutokana na utambulisho wake katika utamaduni wa Kilatino ulimwenguni. Ameunganisha reggaeton, trap, na tamaduni za Kiafrika na Karibiani. Huku akipinga ubaguzi wa rangi kwa kujivunia asili ya Puerto Rico
Mwaka 2026, umeendelea kuwa wa neema kwake kwani ndiye alikuwa msanii wa kwanza kufanya uzinduzi wa Super Bowl Halftime Show kwa kutumia lugha ya Kihispania yote mwanzo mwisho.
Mbali na hayo amewahi kuwa miongoni mwa wasanii waliosikika zaidi duniani kwenye mtandao wa Spotify mara kadhaa. Akikusanya mabilioni ya wasikilizaji duniani. Mbali na muziki, amejikita katika mitindo ya mavazi, filamu, na pia anatumia sauti yake kutetea jamii yake.