Katika mahojiano maalum na UN News, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto na Migogoro ya Silaha, Vanessa Frazier, ametoa tathimini ya ongezeko la kutisha la ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto na umuhimu wa haraka wa kulinda mustakabali wao.

“Kusajili na kutumia watoto vitani bado ni moja ya ukiukwaji ulioenea na wenye madhara makubwa tunayokabiliana nao. Mwaka 2024 pekee, zaidi ya watoto 7,400 waliajiriwa au kutumiwa na majeshi na makundi yenye silaha, na hizi ni kesi zilizothibitishwa tu,” amesema Bi. Frazier, kabla ya siku ya kimataifa ya kupinga matumizi ya watoto kwenye vitai.

“Katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, tumewatenganisha zaidi ya watoto 220,000 kutoka katika makundi yenye silaha,” amesisitiza.

Vanessa Frazier, mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kwa watoto na migogoro ya silaha, ameketi katika studio na nembo ya Umoja wa Mataifa nyuma, akitabasamu wakati wa mahojiano na UN News.

UN News/Charlotte Frantz

Mahojiano na Vanessa Frazier, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kwa Watoto na Migogoro ya Silaha, kwa Habari za UN.

Mgogoro unaoongezeka katika maeneo ya vita

Ofisi yake inafuatilia takribani hali 26 za migogoro duniani, na takwimu zinaonesha hali ya kusikitisha.

“Ukiukwaji huu umeenea zaidi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Nigeria, Somalia, Syria na Myanmar,” ameeleza Bi. Frazier.

“Lakini pia tunaona mwenendo wa kutia wasiwasi nchini Sudan, ambako watoto wanalengwa mahsusi kwa sababu wanaonekana kuwa na manufaa kama walinzi wa mipaka, wafanyakazi, au hata wapiganaji.”

Amesisitiza kuwa nyuma ya takwimu hizo kuna maisha ya watoto yaliyobadilika milele. “Kila namba katika ripoti yetu inawakilisha mtoto ambaye hatimaa yake imekatizwa,” amesema.

Kutoka utekaji hadi kurejea katika jamii

Mbali na kurekodi ukiukwaji wa haki za watoto, ofisi ya Bi. Frazier hushirikiana moja kwa moja na wapiganaji kujadiliana kuachiliwa kwa watoto na kurejea kwao salama nyumbani.

“Moja ya nguvu ya mamlaka yetu ni uwezo wa kujadiliana moja kwa moja na makundi yenye silaha kwa ajili ya kukabidhiwa kwa watoto,” almefafanua. “Baada ya kutenganishwa, UNICEF na washirika wetu hufanya kazi ya kuwaunganisha tena katika jamii, kuhakikisha wanapata msaada wa kisaikolojia, fursa ya elimu na nafasi ya kurejesha utoto wao.”

media:entermedia_image:99bf2304-eb8f-4184-8fe7-90eb35ab81f5

© UNICEF/Roger LeMoyne

Mvulana Mwenye umri wa miaka kumi na moja ameketi katika bweni la kituo cha kuwajumuisha watoto walioachishwa kazi hivi karibuni huko Goma, DR Congo. (Maktaba))

Hata hivyo, kurejea katika jamii mara nyingi hukumbwa na unyanyapaa. “Wasichana wanaorejea huenda wakatengwa na jamii zao, hasa wale wanaorudi na watoto,” amesema. “Kwa sababu za kijamii, baadhi ya wasichana hawawezi kuunganishwa kikamilifu tena na huonekana kana kwamba wameharibiwa.”

Kinga na uwajibikaji

Kwa Bi. Frazier, kinga ndiyo lengo kuu.

“Kinga ni bora kuliko tiba,” amesema. “Ndio maana tunasisitiza kwamba hata wakati wa vita, watoto lazima waendelee kuwa shuleni. Wanapokosa shule, huwa katika hatari kubwa ya kuajiriwa, iwe kwa kulazimishwa au la.”

Pia ameseisitiza kuwa uwajibikaji una nafasi muhimu. Bi. Frazier ambaye awali aliwahi kuwa balozi wa Malta katika Umoja wa Mataifa na mjumbe wa Baraza la Usalama ameelekeza katika mashtaka yaliyofunguliwa katika mahakama za kitaifa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC, kama hatua muhimu za kuzuia uhalifu huo.

“Moja ya zana kubwa za kuzuia ni haki na uwajibikaji,” amesisitiza. “Wakati makamanda wa vita au viongozi wa makundi yenye silaha wanaposhitakiwa na kuhukumiwa kwa kusajili watoto katika mahakama za kitaifa na angalau kesi tatu mbele ya ICC hutuma ujumbe mzito. Inaonesha kuwa uhalifu huu una madhara halisi.”

Imani yake inatokana na uzoefu wa moja kwa moja, kuanzia kukutana na manusura wa utekaji nyara wa Boko Haram nchini Nigeria hadi kusikiliza wanawake waliowahi kufanywa watumwa na Jeshi la Upinzani la Bwana LRA, nchini Uganda.

“Unamsikiliza msichana wa miaka 13 akiwa amembeba mtoto wake, na unatambua jinsi vita vinavyopora utoto wake,” amesema. “Unaposikia hadithi hizi, unatambua kuwa namba katika ripoti zetu ni watu halisi, watoto waliopaswa kuwa na mustakabali mzima mbele yao.”

Msichana mwenye umri wa miaka 13, Elodie, anasimama nyuma ya kamera akiwa ameshikilia silaha bandia, ikiwakilisha safari yake kutoka kuhusishwa na kundi lenye silaha la kupambana na Balaka hadi kurejeshwa na kuingizwa tena Baoro, Jamhuri ya Afrika ya Kati.

© UNICEF/Vlad Sokhin

Elodie, msichana mwenye umri wa miaka 13 ambaye hapo awali alishirikiana na kundi la silaha la kupambana na balaka, anashikilia silaha bandia wakati wa sherehe ya ufunguzi wa kituo cha mafunzo na ukarabati katika mji wa Baoro, Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Watoto ni mfano wa hatia

Bi. Frazier amezungumza kwa hisia kuhusu dhamira yake.

“Watoto ni mfano wa hatia,” amesema. “Hawajachukua upande katika vita vyovyote, lakini hatia na utoto wao vimekatizwa. Watoto hawapaswi kamwe kuchukuliwa kama hasara yakando ya vita.”

Ameongeza kuwa njia ya amani ya kudumu inaanza kwa kuwalinda na kuwawezesha watoto hao hao.

“Uendelevu wa amani unategemea haki za watoto kuendeleza amani hiyo. Wanaporejeshwa kutoka katika migogoro, lazima wapate elimu na nafasi ya kuunganishwa kikamilifu katika jamii, ili waweze kutamani kuwa madaktari, wauguzi, wanasheria, wanasiasa, wahandisi na hilo linawezekana tu kupitia elimu.”

Ujumbe wa matumaini

Mwakilishi huyo Maalum ameeleza kampeni yake ya Prove It Matters, inayowaalika watoto walioathiriwa na vita kutuma ujumbe kwa viongozi wa dunia, uliokunjwa katika umbo la njiwa wa origami ishara ya amani.

“Mtoto mmoja aliniandikia, ‘Bado nina matumaini ya dunia yenye amani. Kamwe tena msichana kuwa mke wa mpiganaji wa msituni. Kamwe tena kuwa sehemu ya makundi yenye silaha. Tuokoe utoto na familia pia.’ Ni ombi la kitoto lisilo na hila, lakini ndilo tunalolipigania,” alisema.

Mvulana mchanga ameketi kitandani mwake katika chumba chenye mwangaza dhaifu kilicho na pazia za zambarau, akitazama nje ya dirisha. Picha hiyo inachukua wakati wa kutafakari, ikiashiria safari yake kutoka utumishi wa kijeshi hadi kurudia elimu na kuota kuwa mfanyakazi wa kijamii.

© UNICEF/Marko Kokic

Kijana na mwanajeshi wa zamani katika mji wa Sultan Kudarat, Ufilipino, ana mpango wa kurudi shuleni.

Mwisho, Bi. Frazier amesisitiza kuwa elimu, haki na matumaini ni nguzo za amani.

“Watoto wanapaswa kuendelea na mustakbali wao hata wakati wa migogoro,” alisema. “Ni suala la kuhakikisha mustakabali endelevu na wa amani kwa dunia.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *