Televisheni ya CNN ya Marekani imefichua malumbano makali ya simu baina ya Rais wa Marekani na Waziri Mkuu wa Israel ambapo Donald Trump amemkemea Benjamin Netanyahu, akimwambia: “Wayahudi wote wamekuchoka,” huku Marekani ikizidisha mashinikizo kwa ajili ya kufikia makubaliano kuhusu Ukanda wa Gaza.

CNN imeeleza kwamba maelezo ya malumbano hayo ya simu, ambayo yalifanyika Septemba mwaka jana, yamesajiliwa katika kitabu cha waandishi wa habari Maggie Haberman na Jonathan Swan, ambao wameyafichua wakati wa mahojiano na mtangazaji wa mtandao wa CNN, Jake Tapper kwenye kipindi cha “The Lead”.

Kwa mujibu wa maelezo ya waandishi hao wa habari, Trump alikuwa akifanya jitihada za kufikia makubaliano kuhusu Gaza, lakini alihisi kwamba Netanyahu hakuwa akishirikiana naye kwa kiwango kinachohitajika.

Trump alimwambia Netanyahu: “Nimechoshwa na matendo yako. Nimefanya kila kitu kukulinda, na bora uendelee na jambo hili la kuchukiza. Kila mtu amekuchoka.”

Trump aliongeza: “Wayahudi wote wamekuchoka, hata Wayahudi walio kwenye mazungumzo haya wamekuchoka,” akimaanisha washauri wake, Jared Kushner na Steve Witkopf.

Mwandishi wa habari wa Israel, Haberman ameendelea kusema: “Shambulio lililofanywa na Israel dhidi ya Qatar lilifanyika wakati Marekani ilipokuwa ikifanya jitihada za kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na kubadilishana mateka huko Gaza,” akiongeza kuwa “hii iliwakilisha hatua ya mabadiliko, hasa katika mtazamo wa maafisa kadhaa wa utawala wa Trump.”

Mwezi Septemba mwaka jana, Israel ilifanya shambulio dhidi ya mji mkuu wa Qatar, Doha, ikilenga ujumbe wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ambao ulikuwa ukijadili pendekezo la Marekani la kusitisha mapigano na kubadilishana mateka katika Ukanda wa Gaza.

Hii si mara ya kwanza kwa Trump, ambaye anafanya jitihada za kusafisha sura mbaya ya Marekani kutokana na kufadhili mauaji ya kimbari ya Gaza, kumkemea Netanyahu hadharani. Mwanzoni mwa Juni, ripoti za vyombo vya habari vya Marekani zilisema kwamba rais wa nchi hiyo alimkemea vikali waziri mkuu wa Israel kuhusu ongezeko la mashambulizi ya kijeshi nchini Lebanon.

Kwa mujibu wa Axios, ikiwanukuu maafisa wa serikali ya Marekani, Donald Trump alimwambia Netanyahu kwa njia ya simu kwamba: “Kama isingekuwa mimi, ungekuwa gerezani hivi sasa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *