Chanzo cha picha, pool via AFP
Muda wa kusoma: Dakika 4
Mapema wiki hii Waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer alipitia wakati mgumu, na labda huenda siku ya Jumatatu ilikuwa siku nzuri kwake.
Waziri huyo alikuwa akipokea shinikizo la kujiuzulu kutoka kwa wadhfa wake, baada ya kulaumiwa kumteua Lord Peter Mandelson kuwa balozi wa Uingereza nchini Marekani, ilhali anahusishwa na Sakata la mnyanyasaji wa kingono Jeffrey Epstein.
Kulikuwa na hofu iwapo wabunge wa chama tawala cha Labour watamshinikiza Waziri huyo mkuu kujiuzulu au kusalia madarakani.
Je, Keir Starmer yuko salama katika wadhfa wake?
Kwa sasa ndio.
Mwakilishi wa Scotland Anas Sarwar, Jumatatu alimtaka Waziri mkuu Starmer kujiuzulu kutoka kwa wadhfa wake, huku maafisa wengine wakitarajia waziri huyo kujiuzulu, wabunge wengi wamesalia kimya.
Baada ya semi za Sarwar za kumtaka Starmer kujiuzulu, naibu waziru mkuu David Lammy, kwenye mtandao wa X alichapisha kuwa Starmer yuko na ‘majukumu makubwa’ ambayo yanafaa kuheshimiwa.
Jumbe sawia kutoka kwa mawaziri na wabunge wa chama cha Labour zilianza kumiminika za kumuunga mkono Waziri huyo mkuu.
Sarwar na Starmer baadaye waliwasiliana kwa njia ya simu ambapo Starmer alimuuliza swali la iwapo atajiuzulu, ni nani atakuwa mridhi wake? Je ni nani ataendeleza sera za chama cha Labour? Na mwelekeo ni upi iwapo atajiuzulu?
Starmer yuko salama kwa muda gani?
Siku ya Jumatatu Starmer alikuwa anapambana kusalia katika wadhfa wake.
Wasiwasi huo umeisha kwa sasa, ila huenda akakumbana na changamoto katika wiki zijazo
Uungwaji mkono ambao Starmer amepokea kutoka miongoni mwa viongozi wa chama cha Labour ni muhimu ila viongozi wengine walifanya hivyo ili kuhifadhi nyadhfa zao.
Ila hii ni hadi mwezi Mwei ambapo taifa hilo litakuwa linafanya uchaguzi wa serikali za mitaa na mabaraza tofauti nchini humo, ambazo huchangia pakubwa uongozi wa serikali kuu.
Wes Streeting anasemaje?
Chanzo cha picha, EPA
Inategemea. Kuna wale ambao wanamuamini Keir Starmer.
Wale wanaomuamini Starmer sasa wanafuatilia kwa karibu anachofanya waziri wa afya Wes Streeting, baada ya kuonyesha nia ya kutaka kuwa waziri mkuu na kuhamia ofisi ya 10 Downing Street.
Watu wengi walimuenzi Streeting baada ya kuchapisha mawasiliano yake ya Whatsapp na Lord Mandelson balozi wa Uingereza nchini Marekani ambaye anatuhumiwa kuwa alikuwa na ukaribu na mnyanyasaji wa kingono Jeffrey Epstein. Streeting alichapisha mawasiliano hayo ili kudhibitisha hana la kuficha na hawana ukaribu na Mandelson.
Streeting ameiambia BBC kuwa bado anamuunga mkono waziri mkuu wa taifa hilo
Aidha mawaziri wengine wametakiwa kutochapisha mawasiliano yao ya Whatsapp na Mandelson.
Streeting pia alikanusha tuhuma kuwa yeye ndiye aliwapatinisha Sarwar na waziri mkuu baada ya mbunge huyo kutaka Starmer kujiuzulu kwa kumteua Mandelson ambaye amehusishwa na sakata la Jeffrey Epstein.
Hapo jana baadhi ya viongozi wa chama cha Labour wanaomuunga mkono Streeting walikuwa wanapania kujiuzulu kutoka serikalini baada ya mkutano wao wa chama cha bunge cha Labour (PLP), ila haikutokea hivyo.
Ila uhusiano kati ya Streeting na waziri mkuu unasemekana kuwa wa mshikemshike.
Wagombeaji wengine ni kina nani?
Chanzo cha picha, PA Media
Majina yaliyotajwa sana na wanachama wa chama cha Labour ni Wes Streeting Waziri wa Afya, Angela Rayner naibu Waziri mkuu wa kitambo, Shabana Mahmood Waziri wa usalama wa taifa, John Healey Waziri wa ulinzi na Ed Miliband Waziri wa nishati.
Wengi waliotajwa na wawakilishi wenza walikuwa wanatajwa kwa maovu yao wala si kufaa kwao kuwa Waziri mkuu.
Hii imechangia pakubwa kwa Starmer kusalia kuwa kiongozi wa chama cha Labour hadi leo.
Je kutakuwa na mabadiliko Downing Street?
Mkuu wa wafanyikazi katika afisi ya waziri mkuu Morgan McSweeney, alijiuzulu siku ya Jumapili, na baadaye kufuatwa na mkurugenzi wa mawasiliano siku ya Jumatatu.
Licha ya baadhi ya wafanyikazi wa waziri huyo kujiuzulu, bado anapokea uungwaji mkono katika chama chake, huku kukikosekana mtu ambaye anaweza kuliziba pengo lake.
Chris Wormald Waziri wa utumishi wa umma pia anatarajiwa kujiuzulu wakati wowote.
Chris alichaguliwa na Starmer mwezi Disemba mwaka wa 2024, na baada ya siku chache tu, maafisa wakuu wa serikali ya Uingereza walianza kutoa malalamishi kumhusu wa iwapo ana uwezo wa kutumikia wizara hiyo.
Ila baada ya watu wengi aliowachagua Starmer kuondoka serikalini, wazri huyo mkuu anasalia na jukumu la kuhakikisha kazi inaendelea kufanyika.
Je, ajenda ya serikali itabadilika?
Edward Miliband Waziri wa nishati wa Uingereza amemtaka Waziri mkuu kuwa na ujasiri na kuegemea sana mrengo wa kushoto
Baadhi ya ajenda za Starmer hazijakaa sawa na wabunge wa Labour, kwani amekua akifanya maamuzi ambayo yameleta mabadiliko makubwa yenye utata.
McSweeney, mkuu wa wafanyikazi aliyejiuzulu ndiye aliyekuwa akinyooshewa lawama wa maamuzi yenye utata, ila sasa macho yanaelekezwa kwa Starmer kuona iwapo anaweza kufanya maamuzi bila ushawishi wa McSweeney.
Ila hii itategemea pakubwa ni nani atachaguliwa kuwa mkuu wa wafanyikazi.
Wabunge wa Chama cha Labour wakishabikia utendaji kazi wa Starmer katika mkutano wa chama siku ya Jumatatu, Waziri huyo mkuu alisema kuwa atapigania kuleta mageuzi nchini humo, na kupigania ‘nchi ninayoipenda’ na hii haibadilishi kuwa kuna uwezekano wa kuibuka kwa sera tofauti haswa katika mfumo wa SEND.
Mbunge mmoja wa chama cha Labour aliyekuwa na mashaka alisema, “Anasema ameshinda kila pambano ambalo amewahi kuwa nalo. Si kweli, amepoteza kila pambano ambalo amewahi kuwa nalo na utendaji kazi katika chama cha bunge cha Labour (PLP). Na hali hiyo haikubaliki.”