Idara ya Ulinzi wa Raia katika Ukanda wa Gaza inasema kuwa maelfu ya miili ya Wapalestina waliouawa katika mashambulizi ya Israel bado imezikwa chini ya magofu ya majengo yaliyoharibiwa katika eneo hilo la Palestina, huku timu za uokoaji zikijitahidi kufika kwenye vitongoji vilivyoharibiwa wakati wa vita vya mauaji ya kimbari vya utawala wa Israel.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa udara hiyo, Mahmoud Basal imesema takriban miili ya watu 8,000 bado iko chini ya vifusi, licha ya juhudi za utafutaji na uokoaji zinazoendelea.

Makundi ya ulinzi wa raia yalionekana yakifanya operesheni kwa kutumia mitambo mikubwa katika eneo la jengo lililoharibiwa wakati wa mashambulizi ya Israel katika kitongoji cha Sheikh Radwan jijini Gaza mnamo Februari 12.

Basal amesema timu za kutafuta miili ya wahanga hao zinafanya kazi chini ya vikwazo vikali. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, timu hizo zinafanya kazi katika “mazingira magumu sana” zikiwa na rasilimali chache, na hivyo kufanya iwe vigumu kufikia maeneo mengi yaliyoathiriwa.

Takwimu za hivi karibuni zimekuja huku taasisi mashuhuri ya sheria za kibinadamu ikionya kwamba idadi ya Wapalestina wa Gaza waliouawa na Israel katika vita vya eneo hilo vilivyoanza Oktoba 2023 inaweza kuwa kubwa zaidi kuliko ilivyoripotiwa.

Chuo cha Sheria za Kimataifa na Haki za Kibinadamu cha Geneva kimesema idadi ya watu waliouawa katika Ukanda wa Gaza huenda imezidi watu 200,000. Tathmini hiyo ilitaja data mpya inayoonyesha kwamba idadi ya watu katika eneo hilo imepungua kwa zaidi ya asilimia 10 tangu kuanzishwa kwa mauaji ya kimbari ya Israel mwaka 2023.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *