
Zanzibar. Rekodi mbili zinaipa matumaini Yanga kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika leo wakati itakapoikaribisha JS Kabylie katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kuanzia saa 1:00 usiku.
Rekodi hizo mbili ni za timu za Al Ahly na FAR Rabat zinazokutana leo huko Cairo, Misri ambazo matokeo yake yana nafasi kubwa kuamua kama Yanga itafuzu robo fainali au safari yake itaishia leo.
Kama ikiifunga JS Kabylie, Yanga itasonga mbele iwapo Al Ahly itapata ushindi wa nyumbani dhidi ya FAR Rabat kwa vile Yanga itafikisha pointi nane na hivyo itapenya kwa kubebwa na utofauti mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Lakini kama FAR Rabat itapata ushindi au sare dhidi ya Al Ahly ugenini, Yanga itaishia katika hatua ya makundi hata kama itapata ushindi dhidi ya JS Kabylie leo.
Rekodi ya kwanza inayoipa matumaini Yanga leo ni ya Ahly kufanya vizuri katika mechi za Ligi ya Mabingwa ambazo inacheza ikiwa nyumbani ambapo katika michezo mitano iliyopita ya mashindano hayo, Al Ahly imepata ushindi mara nne huku ikitoka sare moja tu na imefunga mabao tisa huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili tu.
Ukiondoa hiyo, rekodi nyingine ambayo inaweza kuipa Yanga imani kubwa ya kupenya leo ni ile ya FAR Rabat kutokuwa na makali ugenini pindi inapocheza katika mashindano hayo.
Hilo linaweza kuthibitishwa na mechi tano zilizopita za timu hiyo nje ya ardhi ya Morocco ambapo imeshinda mchezo mmoja tu, ikitoka sare miwili na kupoteza mechi mbili huku ikifunga mabao matatu tu huku yenyewe ikiruhusu mabao sita.
Hata hivyo katika mchezo wa leo, Yanga inapaswa ibadilike zaidi katika safu zake za ulinzi na ushambuliaji ambazo zimeonekana kutocheza vizuri katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Ubutu wa safu ya ushambuliaji ya Yanga umeonekana katika mechi tano ilizocheza kwenye hatua ya makundi ambapo timu hiyo imefumania nyavu mara mbili tu lakini safu yake ya ulinzi imeonyesha udhaifu kwa kuruhusu kufungwa mabao manne.
Ikiwa Yanga itafanikiwa kufuzu, nyota wake watavuna kitita cha Dola 450,000 (Sh1.2 bilioni) kutoka kwa uongozi wa timu hiyo kama ahadi ya kuwahamasisha wafanye vizuri leo.
Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves alisema wanafahamu wapinzani wao hawana presha na mechi kwa sababu hawana nafasi ya kufuzu hivyo kazi ipo juu yao.
“Mechi ngumu na tulijua ugumu wa kundi mapema na tunajua Kablyie hawana nafasi ya kufuzu hivyo tunahitaji kuifikiria zaidi na tunajua hawana presha na hilo lipo kwetu,” alisema Goncalves.
Azam kazi kwao
Wawakilishi wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika, Azam FC leo watakuwa ugenini huko Morocco kukabiliana na Wydad Casablanca katika mchezo utakaoanza saa 11:00 kwa muda wa Tanzania.
Ushindi wa kuanzia mabao mawili au zaidi katika mchezo huo utaifanya Azam itinge katika hatua ya robo fainali.
Na huko Afrika Kusini, wawakilishi wengine wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika, Singida Black Stars watakuwa uwanjani kukabiliana na Stellenbosch, mchezo ambao utaanza saa 1:00 usiku.