
Mmiliki mwenza wa klabu ya Manchester United, Sir Jim Ratcliffe, ameuwasha moto asiokuwa na kazi nao, na sasa unamuunguzia kibanda chake.
Sir Jim Ratcliffe amegonga vichwa vya habari duniani juma hili baada ya kutoa kauli ya kibaguzi dhidi ya wahamiaji nchini Uingereza, iliyowakera wengi.
Akiongea katika mahojiano maalumu na mtangazaji wa kituo cha runinga cha Sky News, Ed Conway, Sir Jim alionesha chuki ya wazi dhidi ya wageni wanaohamia nchini humo akisema wanaibebesha mzigo wa kiuchumi nchi hiyo.
Uingereza imetawaliwa na wahamiaji, hakika, si ndio? Namaanisha, idadi ya watu ya Uingereza ilikuwa milioni 58 mwaka 2020, sasa ni milioni 70. Hao ni watu milioni 12.
Kauli hii imevutia ukosoaji mkubwa kutoka kila kona ya dunia kiasi cha yeye mwenyewe kuomba radhi na kujaribu kuweka upepo sawa.
Hata hivyo kwenye radhi aliyoomba aliendelea kuonesha kibri na ubaguzi kwa kusisitiza msimamo wake dhidi wahamiaji, akisema kitu pekee ambacho labda alikosea ni kuchagua kutumia neno Uingereza kutawaliwa, lakini sio ujio wa wahamiaji.
Kauli yake inaonesha dhahiri kwamba yeye ni mmoja wa watu wasiopenda wageni nchini mwake, na kumuweka kwenye kundi la watu wenye msimamo mkali wa aina hiyo ambao hufanya harakati za kupambana na wahamiaji.
UONGO 1 – IDADI YA WATU
Watu wengi wanaomkosoa, wameanza na uchambuzi wa kimantiki wa kauli yake.
Idadi ya watu ya Uingereza ilikuwa milioni 58 mwaka 2020, sasa ni milioni 70. Ongezeko ni watu milioni 12.
Hapa alidanganya kwani kwa mujibu wa taarifa ofisi ya taifa ya takwimu, Uingereza ilikuwa na watu milioni 66.7 mwaka 2020, sio milioni 58 kama anavyodai.
Na sasa ina watu milioni 69.4, ambalo ni ongezeko la waru milioni 2.7, sio milioni 12 kama alivyodai.
Idadi ya watu milioni 58 anayodai yeye ilikuwa mwaka 1995.
Kwa hiyo ongezeko la watu milioni 12 analodai basi ni la miongo mitatu na ushei.
Tangu 1999 uhamiaji ndio umekuwa chanzo kikuu cha ongezeko la watu nchini humo kuliko hata vizazi.
UONGO 2 – KUTAWALIWA
Uingereza imetawaliwa na wahamiaji, hakika, si ndio?
Kwenye hoja ya kutawaliwa ndio zaidi. Uingereza ndio nchi iliyotawala sehemu kubwa ya dunia kama mkoloni tofauti na anavyodai yeye.
Wahamiaji wanaoingia nchini humo hawaendi kutawala bali kuishi na kufuata sheria za nchi hiyo.
Kutawala au kuwa mkoloni ni kuhamia nchi ya watu, kushika serikali na kuwaongoza watu kimabavu kama ilivyofanya Uingereza yake.
UONGO 3 – KUFAIDIKA BURE
Huwezi kuwa na uchumi wenye kufaidisha bure watu milioni tisa, na wimbi kubwa la wahamiaji likizidi kuja.
Nchi nyingi za Magharibi zina sera ya kusaida watu wasio na kazi au kipato kidogo, kwa kupewa ruzuku na serikali.
Ruzuku hii huitwa BENEFITS. Kwa mashabiki wa muziki hasa wa reggae, wanaweza kulikumbuka kundi la UB40 la Uingereza lililotamba na nyimbo kama Red red wine miaka ya nyuma.
Jina lao, UB40 lina asili ya ruzuku hili ninayotaka kuizunngmzia hapa.
Zamani nchini Uingereza kulikuwa na utatatibu wa kujaza fomu namba 40 kwa watu wasio na ajira, ili wapate ruzuku serikali.
Fomu hiyo ndio iliitwa UB40 ikiwa na maana Un Employment form number 40.
Vijana fulani kutoka jijini Birmingham, wakajaza fomu hiyo na kufaidika nayo.
Baadaye wakaanzisha bendi yao ya muziki na kuiuta UB40 kama kuienzi ile sheria iliyowasaidia.
Sasa sheria hii ndio anayoilalamikia Sir Jim Ratcliffe kwamba inafaidisha bure wahamiaji milioni 9.
Taarifa rasmi kutoka idara ya kazi na mafao inasema watu milioni 10 wa umria wa kuajiriwa ndani ya Uingereza walijaza fomu kuomba ruzuku hiyo Februari 2025.
Hata hivyo, wengi wa waru hawa walikuwa wafanyakazi wa kipato cha chini ambao serikali iliwapa ruzuku kuinua kipato chao kupitia mifuko kama Universal Credit (UC) na ruzuku ya makazi.
Wale waliopokea ruzuku kwa kukosa kazi kabisa walikuwa milioni 6.5, sio milioni 9 kama alivyodai.
Ni kweli idadi imekuwa ikiongezeka kwa siku za hivi karibuni…lakini hata hivyo waombaji sio wageni pekee.
Watu wengi wamemjia juu na kumrushia maneno makali kulaani kauli yake.
Mjini Manchester ambako yeye anamiliki moja ya klabu kubwa, kumewekwa bango kubwa pembeni ya uwanja wa Old Trafford lenye picha ya mchezaji wa zamani wa Manchester United, Marcus Rashford. Picha hiyo imeambatana na maneno makali yanayosema, WAHAMIAJI WAMETOA MCHANGO MKUBWA KWA NCHI HII KULIKO NYIE MABILIONEA WAKWEPA KODI.
Hapa walimlenga Rashford mwenyewe ambaye ni mtu mweusi, kizazi cha wahamiaji anaowazungumzia Sir Jim.
Mwaka 2020 wakati wa UVIKO 19, Rashford alifanya kampeni kubwa na iliyofanikiwa ya kuwasaidia watoto kutoka familia masikini kupata chakula mashuleni.
Kampeni hii ikampa heshima ya kutambuliwa na familia ya kifalme na kupewa cheo cha MBE (Member of the Order of the British Empire).
Wakati Rashford akifanya hivi, Sir Jim na mabilionea wenzake wamekimbilia kuishi Monaco kukwepa kodi kwa sababu nchi hiyo haitozi watu kodi.
Kwa mtindo huo nani ana faida, mzawa kama yeye anayekwepa kodi au mhamiaji kama Rashford anayesaidia watu?
BAO LA KUSAWAZISHA LA PEP
Timu ya Sir Jim Ratcliffe yaani Manchester United iliwafunga 2-0 majirani zao Manchester City wanaofundishwa na Pep Guardiola kutoka Hispania.
Kupitia kauli hii, Pep ni kama ameisawazishia timu yake kwa shuti kali, pale alipotoka hadharani na kulaani, sio tu kauli ya Sir Jim bali tabia ya kuchukia wahamiaji inayoongezeka Ulaya.
Akiongea na vyombo vya habari kuelekea mechi ya Kombe la FA dhidi ya Salford City, Pep alirusha makombora makali sana kwa Sir Jim Ratcliffe na watu wenye filra kama zake.
Duniani kote tatizo ambalo tunalo katika nchi zote (ni kwamba) tunawachukulia wahamiaji au watu wanaotoka nchi zingine kama chanzo cha matatizo ambayo nchi zetu zinayo, na hizi ni tatizo kubwa sana.
Eti kwa kuwa tu mimi ni mkatalunya na wewe ni muingereza – jitihada gani tulikuwa nao hadi tukazaliwa tulipozaliwa? Ni jitihada na mama na baba.
Kila mtu anataka kuwa na maisha bora na mtazamo wa kuwa na kesho bora kwa ajili yao, familia zao na marafiki zao, na wakati mwingine furha huja ulipozaliwa au labda unakoenda.
Hapo kabla ilikuwa vigumu sana kusafiri, lakini leo ndani ya saa moja unaeeza kuwa sehemu yoyote. Leo rangi ya ngozi au wapi ulipozaliwa haileti tofauti yoyote. Tuna kazi kubwa sana ya kufanya kuhusu hilo.
Sir Jim Ratcliffe amezingua pakubwa sana na kauli yake, na dunia imemuonesha kwamba amekosea licha ya kibri chake!