Dar es Salaam. Kati ya wasanii wa Hip-Hop Bongo wanaosifika kuwa na mitindo mingi ya kuwasilisha muziki wao, basi Country Wizzy ni mmoja wapo akiwa na miaka zaidi 15 sasa katika kazi hiyo.
Tayari ana ushawishi wake akiwa ametoa albamu moja, amepita katika makundi na rekodi lebo mbalimbali zenye wasanii wakali, na sasa ana ukurasa mwingine kabisa katika muziki wake. Fahamu zaidi.
1. Country Wizzy alianzisha lebo yake, I Am Music baada ya kuachana na Konde Music Worldwide yake Harmonize ambayo alifanya nayo kazi kwa takribani mwaka mmoja kabla ya kuomba kuondoka.
2. Hapo awali, Country Wizzy na Billnass waliwahi kuwa chini ya rekodi lebo za Rooftop Entertainment, na L.F.L.G (Live First Live Good) ila sasa kila mmoja ana lebo yake inayosimamia kazi zake. Yaani Country Wizzy akiwa na I Am Music, huku Billnass akiwa na Mafioso Inc ambayo tangu 2021 imekuwa ikisimamia miradi yake yote ya sanaa.
3. Ila anadai alipoteza zaidi ya Sh12 milioni katika majukwaa ya kidijitali ya kusikiliza muziki wakati akingojea kukamilika kwa mchakato ya kuhama kampuni iliyokuwa inasambaza muziki wake chini ya Konde Music.
4. Country Wizzy ni msanii wa pili Tanzania kufanya kazi na rapa kutokea Afrika Kusini, Emtee aliyesikika katika ngoma yake, Oright (2023). Wa kwanza Bongo kushirikiana na Emtee, ni Rosa Ree, Way Up (2018).
5. Alishawahi kuwa ndani ya makundi mawili na yote yamevunjika. Kuna kundi la Mtu Chee lililoundwa na wasanii watatu, Country Wizzy, Stamina na Young Dee. Na baadaye kundi la MoCo akiwa na Moni Centrozone.
6. Hata hivyo, Country Wizzy ndiye mwanzilishi wa kundi la Hip Hop la Fresh Boys lenye wasanii wanne, kundi hili analisimamia chini ya lebo yake, I Am Music ambayo aliianzisha 2022.
7. Albamu ya Country Wizzy, Yule Boy (2019) yenye nyimbo 30 ndio albamu ya kwanza ya Hip Hop Bongo kusikilizwa (streams) zaidi ya mara milioni 1 kwenye mtandao wa Audiomack ulioanzishwa 2012. Ikumbukwe rapa J.Cole kutokea Marekani, alikuwa msanii wa kwanza maarufu duniani kutumia mtandao huo, ni pindi alipoweka albamu yake, Yours Truly 2 (2013).
8. Umaarufu wa S2kizzy ulikuja baada ya kutengeneza mdundo wa wimbo wa Country Wizzy, Aah Wapi (2016) ndipo milango ikaanza kufunguka kwa kupata fursa mbalimbali. DJ’s waliupenda sana mdundo huo na wakaanza kuomba wautumie katika kazi zao, na polepole jina la S2kizzy likaanza kusambaa kabla ya kupata nafasi ya kufanya kazi katika studio ya Quick Rocka, Switch.
9. Jina maarufu la S2kizzy ‘Zombie’, hilo alipewa na Country Wizzy ambaye alikuwa anapenda kulitaja katika nyimbo zake alizotayarisha ila Diamond Platnumz ndiye amekuja kulikuza zaidi jina hilo.
10. Country Wizzy na S2kizzy walisafiri kwenda Nairobi, Kenya ili kushuti video ya wimbo wao, Wanaona Haya (2018) ambao walimshirikisha Khaligraph Jones ambaye alitaka wamfuate huko kwa sababu zake binafsi.