
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), Rafael Grossi wamekutana katika jiji la Geneva nchini Uswisi, kabla ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Araghchi na Grossi wamejadili masuala ya kiufundi yanayohusiana na ushirikiano wa Tehran na IAEA katika mfumo wa ushirikiano wa ulinzi na sheria ya Bunge la Iran kuhusu suala hilo.
Kadhalika, mitazamo ya kiufundi ya Iran kuhusu mazungumzo yake yasiyo ya moja kwa moja na Marekani pia ilijadiliwa.
Mkutano wa leo Jumatatu umekuja huku Iran na Marekani zikitarajiwa kufanya duru ya pili ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kuhusu mradi wa nyuklia wa amani wa Jamhuri ya Kiislamu kesho Jumanne. Oman inatarajiwa kuendelea na jukumu lake la upatanishi kwenye mazungumzo hayo ya kesho.
Wakati huo huo, Sayyid Araghchi amekosoa tena vitisho vya Washington dhidi ya Iran, akisema safari yake kwenda Geneva kufanya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani inalenga kufikiwa makubaliano ya haki na usawa.
“Niko Geneva na mawazo halisi ya kufikia makubaliano ya haki na usawa. Kile ambacho hakipo mezani, ni kujisalimisha mkabala wa vitisho,” Araghchi ameandika katika ujumbe alioutuma kwenye akaunti yake ya X baada ya kuwasili katika jiji la Uswisi leo Jumatatu.
Huku hayo yakiarifiwa, Ali Larijani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesema kwamba Tehran iko tayari kwa mazungumzo ya haki ya nyuklia ambayo yatapatia ufumbuzi wasiwasi uliopo.
Dakta Larijani amesema hayo katika mahojiano yake na televisheni ya Al Jazeera na kuongeza kwamba: Iran haijatoa jibu lolote la maandishi kwa matakwa ya Marekani, lakini kubadilishana mitazamo bado kunaendelea.
Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameeleza kuwa, nchi za eneo hili la Asia Magharibi zinaunga mkono kufikiwa suluhisho la kisiasa kwa suala la nyuklia la Jamhuri ya Kiislamu.
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameongeza kuwa: Mazungumzo yetu yanaihusu Marekani pekee – hatushiriki katika mazungumzo yoyote na Israel.