
Ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis imebaini kuwa zaidi ya theluthi moja ya watu hao sasa wanafikiria kukimbilia nje ya nchi tena kutokana na hali mbaya ya maisha.
Mkurugenzi Mkuu wa IOM, Amy Pope, ametoa angalizo leo kutokea jijini Geneva na Kyiv, akisema takriban raia 325,000 wa Ukraine waliorudi nyumbani wako hatarini kukimbia makazi yao kwa mara ya pili. Amy Pope amesisitiza kuwa uvumilivu pekee hauwezi kuzisaidia familia kupita katika kipindi kingine cha baridi kali na giza.
“Baada ya miaka minne ya vita, uvumilivu pekee hauwezi kuzisaidia familia kupita kipindi kingine cha baridi kali na kukatika kwa umeme. Nyumba salama, nishati ya uhakika, na huduma muhimu si mambo ya anasa, ni misingi ya usalama, maisha, na utu wa watu”, amesisitiza.
Hadi kufikia mwezi Januari mwaka huu, Ukraine imekuwa na wakimbizi wa ndani milioni 3.7, huku zaidi ya watu milioni 4.4 wakiwa wamesharejea makwao tangu vita iongezeke.
Baridi kali ya nyuzi -20 inatesa familia
Hali ya baridi imeshuka hadi kufikia nyuzi joto hasi -20°C, jambo linalosababisha mahitaji makubwa ya vifaa vya kuzalisha umeme na majiko ya joto. Katika maeneo mengi ambayo vita imepamba moto, uhitaji wa vifaa kama jenereta na vifaa vya kurekebisha nyumba umefikia asilimia 90, jambo ambalo limekuwa likizidisha msongo wa mawazo kwa familia nyingi. Wale waliorudi hivi karibuni wameonekana kuathirika zaidi, huku wengi wakilazimika kutumia mbinu ngumu za kimaisha ili tu kupata mlo na joto la kuwahifadhi wasigande kwa baridi kali.
Tangu mwaka 2022, shirika la IOM limekuwa likitoa msaada kwa watu milioni 6.9 ndani ya nchi na mamilioni ya wengine katika nchi 11 jirani, lakini mahitaji bado ni makubwa. Kupitia ushirikiano na wadau zaidi ya 270, shirika hilo limekuwa likipambana kuunganisha msaada wa dharura na mipango ya muda mrefu ya kurejesha maisha ya kawaida. Hata hivyo, bila msaada endelevu kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, kukatika kwa nishati kumeendelea kutishia juhudi zote za kurejesha watu makwao na kunaweza kusababisha wimbi jipya la wakimbizi kwenda nchi za nje.
Shirika la IOM limehimiza Jumuiya ya Kimataifa kusaidia katika ukarabati wa nyumba, kutoa msaada wa kisaikolojia, na kuimarisha mifumo ya nishati hasa katika maeneo yanayokabiliwa na vita. Ni wazi kuwa bila msaada wa haraka na wa kutosha, baridi kali na giza vinaweza kufuta matumaini yote ya raia waliojaribu kuanza maisha mapya nyumbani kwao nchini Ukraine.