
Ismail Baqaei Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa Tehran imeingia katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani kwa mtazamo wenye mwelekeo wa matokeo, huku ikibainisha shaka kuhusu taarifa zinazokinzana za Washington.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza haya jana alipozungumza na shirika la habari la IRNA muda mfupi kabla ya ujumbe wa Iran kuondoka Tehran kuelekeza nchini Uswisi.
Baqaei amesema: Kile kinachoitatiza Iran ni kubadilika misimamo na kutolewa kauli zinazokinzana; si tu kutoka kwa wapatanishi bali pia kutoka kwa maafisa wa Marekani.
“Wanatuma ishara na jumbe zisizo na uwiano kabisa, ambazo hazionyeshi uzingatiaji wowote. Iran inajadiliana “katika hali ya kutoaminiana kabisa na ya mashaka, na haiwezi kupuuza tajiriba yake ya huko nyuma hata kidogo,” amesema Ismail Baqaei.
Jumbe za Iran na Marekani, zikiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi na Mjumbe Maalum wa Marekani Steve Witkoff, zilianza mazungumzo ya nyuklia huko Muscat Februari 6, miezi kadhaa baada ya uvamizi wa kijeshi wa Israel dhidi ya Iran mwezi mwaka jana.
Duru ya pili ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani inafanyika mjini Geneva kwa upatanishi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman katika ubalozi wa Oman.
Wakati mivutano kati ya Iran na Marekani ikizidi kuongezeka, Tehran imesisitiza kuwa, machaguo yake yote yako mezani, licha ya mazungumzo yanayoendelea baina yake na Washington.
Kwa mujibu wa Pars Today, sambamba na kushtadi mivutano kati ya Iran na Marekani na kuongezeka kiwango cha vitisho vya kijeshi vinavyotolewa na Washington, Tehran imesisitiza kuwa, licha ya kuendelea mazungumzo, machaguo yote yako mezani, kuanzia utumiaji wa makombora yake hadi ufungaji wa Lango-Bahari la Hormuz.