DAR ES SALAAM: WAJASIRIAMALI wanawake bado wana fursa ya kukuza mitaji, na kutunza fedha zao kupitia akaunti maalumu ya Waridi ya
Benki ya Akiba Commercial Bank (ACB).

Akizungumza jana, Meneja wa ACB Tawi la Mbagala, Adelina Mzelela alisema benki hiyo inatambua umuhimu wa wanawake katika jamii na jukumu lao katika maendeleo ya uchumi, hivyo uanzishwaji wa bidhaa hiyo jibu la kukuza uchumi wa wanawake.

“Akaunti hii inatoa urahisi na ufanisi, bila ada ya kila mwezi akaunti inaweza kufunguliwa kwa shilingi za Tanzania au dola za Marekani, ikifanya iweze kupatikana kwa wigo mpana wa wateja,” alisema.

Akaunti ya WARIDI imeundwa ili kusaidia wafanyabiashara wanawake kuokoa pesa zao na kupata huduma za benki za kidijitali kama vile Akiba Mobile na Wakala, ambazo zinawawezesha kufanya shughuli za benki wakati wowote na popote.

Aidha, kwa upande wake, Dora Saria, Mkuu wa Masoko na Mawasiliano, alisisitiza kuwa elimu ya fedha ni kipaumbele cha kimkakati kinacholenga kuiwezesha jamii kuwa na uelewa wa maswala ya akiba, ukopaji na uwajibikaji, huduma za kifedha za kidijitali, fursa za uwekezaji na mbinu bora za usimamizi wa fedha.

Aliongeza kuwa kwa kukuza utoaji wa Elimu za Fedha na kuhimiza matumizi makini ya huduma za kibenki jamii itaweza kunufaika kiuchumi na kimaendeleo.

Alibainisha zaidi kuwa kadiri taswira ya kifedha nchini Tanzania inavyobadilika, hasa kupitia kuongezeka kwa matumizi ya kidijitali, umuhimu wa elimu ya kifedha unaongezeka sambamba na mabadiliko hayo na hivyo kupelekea kuongezeka kwa juhudi na kipaumbele cha kuelemisha jamii katika uelewa wa Elimu ya Fedha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *