
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Wizara ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuchochea ukuaji wa uchumi.
Amesema ushirikiano huu unatoa fursa ya kupata ufumbuzi wa haraka kwa changamoto zinazojitokeza katika masuala ya Muungano hususan katika upatikanaji wa mikopo kutoka taasisi za fedha za kimataifa. Dk. Mwinyi ameyasema haya wakati alipokutana na Waziri wa Fedha Balozi Khamis Mussa Omar aliyeambatana na watendaji wakuu wa Wizara, katika Ikulu Zanzibar, leo tarehe 18 Februari 2026.

Rais Dk. Mwinyi amesisitiza Zanzibar inaridhishwa na mwendelezo wa vikao vya pamoja vinavyolenga kutatua changamoto za masuala ya Muungano na kuhimiza kuwepo kwa utaratibu bora zaidi unaoinufaisha pande zote. Aidha ameishauri Wizara ya Fedha kuendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuhakikisha masuala ya Muungano yanashughulikiwa kwa ufanisi, uwazi na manufaa ya pande zote.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Khamis Mussa Omar amemuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kuwa Wizara yake itaendelea kutoa ushirikiano wa kiwango cha juu na kutumia kikamilifu fursa za kifedha na kiuchumi ili kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Zanzibar na Tanzania Bara. SOMA: TRA yaagizwa kukomesha matumizi mabaya ya misamaha ya kodi nchini