Dar es Salaam. Mwigizaji na mtayarishaji wa filamu nchini, anayefahamika zaidi kupitia filamu ya Going Bongo, Ernest Napoleon, amesema kuna vitu vingi vya kurekebisha katika kiwanda cha filamu Bongo.
Akizungumza na waandishi wa habari, leo Februari 18,2026 wakati akitambulisha tamthilia yake mpya iitwayo ‘Nipo Bongo’ inayoruka kupitia jukwaa la mtandaoni Bongolix. Ernest amesema kiwanda cha filamu kinakwamishwa na baadhi ya watu wanaopenda vitu vya mkato.
“Kuna vitu vingi vya kurekebisha Bongo. Nilikuwa kwenye tuzo, nikaona Best Series za Afrika Mashariki zote ni Uganda na Kenya. Inaonesha jinsi gani tulivyo nyuma, lakini siyo kwamba sisi ni wajinga.
Kushoto ni mkurugenzi wa BongoLix, Kabenda Balete , katikati mwigizaji na mtayarishaji wa filamu nchini Ernest Napoleon,
“Ni kwa sababu tuna ‘shortcut’ nyingi kuanzia kwenye bajeti, stori, hadi uigizaji. Hiyo ni tofauti kubwa kati ya sisi na wenzetu, wao wanafanya kazi bajeti ipo juu. Wanazingatia uandishi kazi ikitoka inakuwa na ubora,”ameeleza Ernest
Aidha ameongezea kuwa hilo linajionesha hata akiwa location, baadhi ya wasanii wapo nje wa muda hadi wapigiwe simu ndiyo hufika.
“Kwa Tanzania hapa, nikifika ‘seti’ naanza kuwapigia wasanii simu. Kwa hiyo ni moja ya tofauti inayodumaza, tumeishia kutafsiri movie za wenzetu ambao kiuhalisia hawajatuzidi,”amemalizia Ernest
Mkurugenzi wa BongoLix, Kabenda Balete akizungumza na waandishi wa habari. Februari 18,2026
Hata hivyo kwa upande wake Kabenda Balete, Mkurugenzi wa BongoLix jukwaa la kuangalizia movie, amesema maono ya kutengeneza Bongolix ni kuhakikisha kuwa jukwaa ambalo linamilikiwa na Watanzania.
“Watanzania wanaoangalia filamu kwenye Bongolix ndiyo wanatupa hamasa. utandawazi unakua kwa kasi kuangalia kazi kwenye TV kunapotea taratibu DVD ndiyo hizo zimeondoka Miaka inavyoenda ndivyo hivyo Watanzania wengi wanatamani kupata maudhui kwenye simu zao.
“Lengo letu sisi ni kuhakikisha kunakuwa na uwazi mtu anaweza, kutengeneza filamu yake akaja kuisambaza kwetu tunampa nafasi ya kuwa anaona mapato yake. Na wengine tunashirikiana nao kama tulivyoshirikiana na Napoleon. Tunahakikisha vijana wanaweka nguvu katika vipaji vyao na wanapata masoko. Kuna masoko ya ndani na nje,”amesema na kumalizia.
“Jukwaa letu tunataka kujikita na lugha ya Kiswahili, tunaamini lugha yetu inaweza kuwa kinara. Pia kupeleka elimu kwa njia ya filamu kwenye masoko ya Kimataifa, lengo ni kusaidiana na prodyuza, waandishi kuzalisha kazi ambazo ni bora kwa kutumia wataalamu wa ndani ili kukuza vipaji,”amesema Kabenda
Ikumbwe tamthilia ya ‘Nipo Bongo’ inaoneshwa kupitia jukwaa la Bongolix ambalo hupakuliwa kwenye simu janja. Hadi sasa zimeachiwa episodi mbili za tamthilia hiyo huku ndani wakiwemo waigizaji maarufu akiwemo Isarito Mwakalindile