
Spika wa Bunge la Iran amesisitiza tena kwamba atatetea haki za Wairani waliouawa shahidi wakati wa mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu baada ya kuwasili Uswisi kufuatilia mkataba wa Hati ya Maelewano uliosainiwa na viongozi wa nchi mbili kwa lengo la kukomesha vita.
Mohammad Baqer Qalibaf amesema hayo katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X alipowasili Zurich kwa mazungumzo ya jinsi ya kutekeleza yaliyomo kwenye hati ya makubaliano hayo, ambayo yalitiwa saini hivi karibuni kati ya marais wa Jamhuri ya Kiislamu na Marekani.
“Ninawaona watoto wasio na hatia wa Minab na mashahidi wote wa Iran yetu tunayoipenda kama mashahidi wanaotazama matendo na mwenendo wangu daima,” ameongeza Qalibaf, akiashiria mji wa Minab kusini mwa Iran, ambapo watoto 168 wa shule ya msingi na walimu wao zaidi ya 25, waliuawa shahidi baada ya Marekani na utawala wa katili wa Israel kushambulia shule yao tarehe 28 Februari.
“Wanatuona na wana matarajio kutoka kwetu,” amesema Spika wa Bunge anayeongoza ujumbe wa Iran kwenye mazungumzo ya Uswisi na kuongeza kuwa: “Mungu akipenda, sitaaibika mbele ya mashahidi wasio na hatia na watu wa Iran.”
Ujumbe huo umeambatana na picha ya Spika Mohammad Qalibaf alipokuwa akishuka kutoka kwenye ndege iliyobeba ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ambao umepewa jina la “Minab 168” kwa ajili ya kuwakumbukka mashahidi wa shule hiyo.
Ujumbe huo, ambao unajumuisha Waziri wa Mambo ya Nje, Abbas Araqchi, unatarajiwa kufanya majadiliano na Wamarekani kuhusu jinsi ya kutekeleza majukumu yaliyokubaliwa na pande hizo mbili kwenye Hati ya Maelewano.