
KOCHA Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves amesema kutakuwa na mabadiliko ya mara kwa mara kwenye kikosi cha timu hiyo kutokana na ratiba ngumu iliyo mbele yao, huku akiwaonya wachezaji wa kikosi hicho kuacha kuridhika wapatapo nafasi, akisisitiza kila mmoja anapaswa kuonyesha kitu pindi akiaminiwa.
Wakati huohuo amezungunzia kutokuonekana kwa Clement Mzize licha ya kupata nafasi ya kucheza dakika chache dhidi ya AS FAR Rabat katika Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi akisema bado hajawa fiti, hivyo wanasubiri majibu ya mwisho ya vipimo kama atatakiwa kuendelea kutumika.
Amefunguka hayo baada ya Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cosmopolitan katika hatua ya 64 Bora ya Kombe la Shirikisho (FA) iliyochezwa Februari 18, 2026 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar.
Baada ya mechi hiyo, timu imepewa mapumziko ya siku moja na inarejea kambini leo Ijumaa tayari kwa maandalizi kabla ya Jumamosi kuanza safari ya kuifuata Namungo kwa ajili ya mechi ya Ligi Kuu Bara itakayopigwa Jumapili, Februari 22 mwaka huu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Pedro alisema wachezaji waliocheza wamepata kipimo kizuri kutoka kwa wapinzani kwani ulikuwa mchezo mzuri kutokana na Cosmopolitan kujiandaa vizuri kuonyesha ushindani, huku akilia na wachezaji wake kukosa mwendelezo mzuri wa ubora.
“Licha ya timu kupata matokeo, lakini haikuwa vizuri kama tulivyokuwa tunatarajia, mchezaji hata asipopata mechi mara kwa mara kile anachokipambania akiwa katika uwanja wa mazoezi anatakiwa kukionyesha kwenye mechi ya ushindani ili kunipa nafasi ya kumuamini zaidi, wengi wamecheza kawaida, hii siYo nzuri.
“Tuna mechi nyingi na ratiba siyo rafiki kwetu, ni muda wa wachezaji ambao hawajapata nafasi ya kucheza huku wengine wakitumika mara kwa mara kwa mechi ngumu tulizocheza za Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo tunawapumzisha ili kurudisha utimamu kabla ya kumkabili mpinzani wetu Simba,” alisema Pedro.
Alisema kila mchezaji aliyesajiliwa Yanga ana umuhimu wake na atatumika kulingana na mahitaji ya mechi husika, hivyo anaheshimu uwezo wa kila mmoja lakini anawakumbusha kuipa thamani hata dakika moja wanayoipata kuitumikia timu hiyo ambayo ina malengo makubwa msimu huu.
MZIZE BADO, PACOME FRESH
Kuhusu Mzize ambaye alikuwa nje ya uwanja kwa takribani miezi minne kabla ya kurejea Februari 7, 2026 akitokea benchi dhidi ya AS FAR Rabat, Pedro alisema Mzize bado anaendelea kufuata maagizo ya daktari juu ya namna ya kujiweka katika hali ya utimamu na wao kama benchi la ufundi wanasubiri majibu ya MRI kujua kama amerudi katika kiwango chake ambacho kitamfanya amtumie kikamilifu.
“Nafikiri wengi wanajiuliza ni kwa nini Mzize hatumiki, wafahamu bado anaendelea kupona jeraha lake, nafikiri siku mbili tatu zijazo klabu itatoa majibu ya vipimo vyake kwani tayari amefanyiwa MRI.
“Mzize ni mchezaji mzuri na tayari alishaanza kurudi uwanjani ndiyo maana tulimpa dakika chache za kucheza lakini mambo bado hayapo sawa upande wake, majibu ya kipimo cha mwisho yatatoa picha ya siku gani atarudi uwanjani moja kwa moja kuendelea kuipambania Yanga.
“Kuhusu Pacome Zouzoua hajapata shida kubwa, zaidi nimempa muda wa kupumzika, ili aweze kupata nafasi ya kurudi katika utimamu baada ya kutumika muda mrefu ukiondoa dakika nyingi kiwanjani, pia safari za mara kwa mara, hivyo anatakiwa kupata mapumziko sio yeye pekee ni wachezaji wengi waliofanya kazi kubwa kila mmoja atapata nafasi kwa wakati wake,” alisema Pedro.
Yanga inayoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 22 baada ya kucheza mechi nane, itacheza dhidi ya Namungo (Februari 22), kisha JKT Tanzania (Februari 25) kabla ya Machi Mosi kuikaribisha Simba katika Dabi ya Kariakoo itakayochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.