WAKATI mshambuliaji wa Simba, Jonathan Sowah akiwekwa kando katika majukumu yanayoendelea ya msimu huu, taarifa mpya inayomhusu staa huyo ni kwamba kuna asilimia 80 za kurejea tena Singida Black Stars.

Sowah Alijiunga na Simba Januari 08/2025 akitokea Singida Black Stars ambako alifunga mabao 13 baada ya kusajiliwa dirisha dogo kutoka Al-Nasr ya Libya.

Viongozi wa Singida BS walitoa taarifa za Sowah kumtoa bure kwenda Simba ambako hadi sasa amefunga mabao matatu kabla ya kuweka nje ya kazi, sababu ikitajwa ni kutokana na matatizo ya kinidhamu.

Mwanaspoti lilipata taarifa ya ndani kutoka Singida BS, kuwepo kwa mazungumzo na Sowah ili kurejea kwao msimu ujao.

“Sowah anawasiliana moja kwa moja na kiongozi wa juu kabisa, asilimia ni kubwa kuwepo kikosini msimu ujao, ingawa ni mchezaji lolote linaweza likatokea kwake endapo akipata sehemu ya maslahi zaidi,” alisema kiongozi huyo na kuongeza;

“Mbali na mambo mengi yanayosemwa kuhusu Sowah kama utovu wa nidhamu, lakini ni mchezaji mzuri sana akijengwa, ndiyo maana alifunga mabao 13 kwa kipindi kifupi, naamini Simba angecheza mechi nyingi huenda angekuwa anaongoza kwa mabao.

“Kabla ya kwenda Simba timu ya kwanza ambayo ilikuwa inafukuzia saini yake akiwa Singida BS ilikuwa ni Yanga, mambo yakienda sawa tunaamini Sowah atafanya vizuri.”

Staa wa zamani wa Simba, Steven Mapunda ‘Garincha’ alisema:”Inahitaji uvumilivu na saikolojia kubwa jinsi ya kukaa na wachezaji ambao wamelelewa malezi tofauti, mfano kama Sowah  ni mchezaji mzuri sana, sasa inatajwa nidhamu ndio tatizo, wachezaji wakubwa duniani wengine ni watukutu lakini wamewawekea watu wakuzungumza nao.”

Mtaalamu wa Saikolojia Charles Nduku alisema:”Kuna umuhimu mkubwa wa klabu kuwa na wataalamu wa saikolojia ambao watasaidiana na makocha au wawe na watu maalumu wa kuzungumza na wachezaji wao mara kwa mara, kama wanavyofanya Ulaya, asilimia kubwa wachezaji wengi wana vipaji lakini nidhamu ndogo, hilo linatokana na mambo mengi inaweza ikawa vitu vipya kuingia maisha mwake ambavyo hakupewa elimu kabla.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *