Dar/Arusha. Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Tabora imefuta utaratibu wa wanasheria wanaofanya kazi katika sekta za umma kupewa hadhi ya uwakili, bila kupitia mafunzo ya uwakili katika Shule ya Sheria Tanzania (SLT), utaratibu ambao mawakili wamekuwa wakiuita ‘uwakili wa viti maalumu’.

Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kubatilisha vifungu vidogo (2) na (3) vya kifungu cha 2 cha Sheria ya Shule ya Sheria Tanzania [Sura ya 425 Toleo la 2023] na Kanuni za Shule ya Sheria Tanzania (Msamaha kwa Maafisa Fulani), Tangazo la Serikali Na. 839 la mwaka 2023.

Uamuzi huo uliotolewa Februari 17, 2026, unatokana na uamuzi wa wengi katika shauri la kikatiba lililofunguliwa na Amina Moshi Mwaluko dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), lililosikilizwa na jopo la majaji watatu– Adamu Mambi (mwenyekiti wa jopo), Dk Zainabu Mango na Dk Frank Mirindo.

Amina ni mhitimu wa Shahada ya Sheria wa mwaka 2010 kutoka Chuo Kikuu cha Zanzibar na Katibu Mwandamizi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (Tughe), mkoa wa Tabora.

Katika shauri hilo alipinga uhalali wa kikatiba wa masharti ya vifungu vidogo (2) na (3) vya kifungu cha 2 cha Sheria ya Shule ya Sheria Tanzania [Sura ya 425 Toleo la 2023] na Kanuni za Shule ya Sheria Tanzania (Msamaha kwa Maafisa Fulani), Tangazo la Serikali Na. 839 la mwaka 2023.

Kwa vifungu hivyo, Jaji Mkuu anaweza, kwa maombi, kumsamehe ofisa sheria yeyote, ofisa wa mahakama wa cheo cha ofisa mwandamizi au zaidi, na mwanasheria yeyote mwenye sifa anayefanya kazi katika utumishi wa umma mwenye cheo kinacholingana na wakili wa Serikali mwandamizi au zaidi, ambaye anazo sifa za kitaaluma zilizowekwa katika kifungu cha 8(1)(a) cha Sheria ya Mawakili.

Pia, Jaji Mkuu anaweza kutunga kanuni zinazoelekeza utaratibu na namna ya kuomba msamaha, uzoefu wa vitendo unaohitajika kwa ajili ya msamaha, na namna ya kuchambua maombi hayo, ambapo Jaji Mkuu alitunga Kanuni za Shule ya Sheria Tanzania (Msamaha kwa Maafisa Fulani), Tangazo la Serikali Na. 839 la mwaka 2023.

Kanuni ya 3(b) inaongeza sharti la kuwa na uzoefu wa vitendo wa miaka 10 katika masuala ya sheria kama mojawapo ya masharti ya chini ya kupata msamaha wa kisheria.

Mahakama hiyo, baada ya kusikiliza hoja za pande zote katika uamuzi wake, majaji walio wengi, yaani Dk Mango na Dk Mirindo, wamekubaliana na hoja za mdai na kubatilisha vifungu hivyo baada ya kuridhika kuwa vinakiuka Katiba ya nchi kwa kuwa vinaweka ubaguzi.

Hata hivyo, Jaji Mambi ametofautiana na majaji walio wengi na kuandika hukumu yake ya kutofautiana na wenzake ambapo ametupilia mbali madai na hoja za mdai, akikubaliana na hoja za mdaiwa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuwa vifungu hivyo haviweki ubaguzi.

Hata hivyo, uamuzi wa wengi ndio unaofanya kazi, isipokuwa kama utabadilishwa na Mahakama ya Rufani.

Msingi wa madai na hoja za Amina

Amina alidai vifungu vidogo hivyo na kanuni zake ni batili kwa kuwa vinakiuka haki ya usawa mbele ya sheria kama ilivyoainishwa katika Ibara za 12 na 13(1), (3), (4) na 22(2) za Katiba ya nchi ya mwaka 1977.

Alidai kuwa masharti hayo yanawanyima msamaha huo wahitimu wengine wa sheria wenye sifa sawa na hao kwa sababu tu ya mahali walipoajiriwa.

Alieleza kuwa, ingawa amesajiliwa kama wakili Zanzibar tangu mwaka 2019, lakini mwaka 2025 alikataliwa maombi ya kusajiliwa katika Dafatari la Mawakili licha ya kuwa na sifa nyingine zote zinazohitajika chini ya mfumo wa msamaha wa kisheria, kwa sababu hajapitia mafunzo ya vitendo katika Shule ya Sheria Tanzania.

Alidai kwamba kukataliwa huko kumemnyima fursa sawa ya kufanya kazi kama wakili Tanzania Bara, kama ilivyo kwa mawakili waliopata msamaha katika sekta ya umma, jambo ambalo limemuathiri yeye binafsi, mwajiri wake (Tughe), wanachama wa Tughe na umma kwa ujumla.

Mawakili wa Amina walidai kuwa masharti hayo yanakinzana na lengo la kikatiba chini ya Ibara ya 9(1)(h) la kuondoa aina zote za ubaguzi, kama linavyoakisiwa katika masharti yanayotekelezeka ya Ibara za 12(1) na 13(1).

Hivyo, waliiomba Mahakama itangaze masharti hayo kuwa ni batili kwa kukiuka Katiba.

Amina aliwakilishwa na mawakili– Mugaya Kaitila Mtaki, Akram William Magoti Juma, Kamaliza Kamoga Kayaga, Kelvin Kayaga na Fadhili Kingu.

Majibu ya hoja za Serikali

Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika majibu yake wakati wa usikilizwaji kupitia Wakili wa Serikali Mwandamizi, Stanley Kalokola, alidai kwamba masharti yanayopingwa ni ya udhibiti tu na si ya kuzuia, na kwamba mawakili wasiostahili msamaha bado wanaweza kuhudhuria mafunzo ya vitendo katika Shule ya Sheria Tanzania.

Wakili Kalokola alidai kuwa masharti hayo hayahusiani na haki ya ajira au haki ya kufanya kazi, bali yanadhibiti sifa za kitaaluma kwa ajili ya kufanya kazi ya uwakili Tanzania kwa wale wanaostahili msamaha kabla ya kuandikishwa katika Daftari la Mawakili.

Aliongeza kwamba lengo la Shule ya Sheria Tanzania la kutoa mafunzo ya vitendo chini ya kifungu cha 5(a) cha sheria iliyoianzisha, linatimizwa na maofisa waliosamehewa ambao wamepata “uzoefu wa vitendo” wakiwa katika utumishi wa umma.

Uamuzi wa Mahakama (walio wengi)

Jaji Dk Mango na Dk Mirindo katika uamuzi wao, pamoja na mambo mengine, wamesema kuwa sheria ni taaluma inayotegemea sifa na umahiri, na mfumo wake wa kuthamini sifa lazima uendane na kanuni ya usawa mbele ya sheria.

Wamebainisha kuwa shauri hilo lilijengwa juu ya Ibara za 12, 13(1), 13(2) na 13(4), ambazo kwa pamoja zinahakikisha usawa wa binadamu wote, heshima ya utu, usawa mbele ya sheria na kanuni ya kutobagua.

Wamesema kuwa ni dhahiri kuwa vifungu vinavyopingwa vinabagua kwa namna isiyo ya uwiano kati ya mawakili wa sekta binafsi na umma, kwa kurahisisha njia kwa mawakili wa sekta ya umma kuwa mawakili wa kujitegemea kwa gharama ya rasilimali za umma, huku wakinyima fursa kama hiyo wale wa sekta binafsi.

Kwa sababu zilizotajwa hapo juu, wamesema kuwa shauri hilo linaruhusiwa na kusema:

“Inaamriwa kwamba vifungu vya 2(2) na 2(3) vya Sheria ya Shule ya Sheria Tanzania [Sura ya 425 Toleo la 2023], kama vilivyorekebishwa na kifungu cha 43 cha Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) Sheria Na. 6 ya 2020 pamoja na Kanuni zake zijulikanazo kama “Law School of Tanzania (Exemption of Certain Officers) Rules, GN Na. 839 ya 2023,” vinakiuka masharti ya Ibara ya 12 na 13(1), (2) na (4) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.

“Vinatangazwa kuwa batili kuanzia tarehe ya uamuzi huu na kuendelea. Aidha, vifungu hivyo havina tena nguvu za kisheria na vinafutwa mara moja kutoka katika vitabu vya sheria,” imesisitiza Mahakama.

Uamuzi wa Jaji Mambi

Jaji Mambi katika uamuzi wake, baada ya kujadili hoja za pande zote pamoja na mambo mengine, ameeleza kuwa maofisa wa sheria wa umma wanaosamehewa chini ya vifungu vinavyolalamikiwa si kwamba wanapewa upendeleo wa moja kwa moja, bali hupitia utaratibu maalumu unaohusisha uchunguzi wa sifa, uzoefu na uadilifu wao kabla ya kuruhusiwa kuandikishwa.

Jaji Mambi amerejea kumbukumbu za majadiliano ya Bunge (Hansard), akieleza kuwa marekebisho hayo yalilenga kuzingatia uzoefu wa vitendo wa maofisa wa umma waliokuwa wanatekeleza majukumu ya kisheria kwa muda mrefu.

Amesisitiza hayakulenga kubagua wanasheria binafsi, bali yalikuwa hatua ya sera ya kuoanisha sheria na kutambua uzoefu wa kitaaluma uliopatikana kupitia utumishi wa umma.

“Nia ya Bunge haikuwa kubagua, bali kuoanisha sheria na kutambua uzoefu wa vitendo walioupata maofisa wa umma katika utumishi wao,” ameeleza.

Ametahadharisha kuwa mahakama inapaswa kuchukua tahadhari kubwa kabla ya kubatilisha sheria iliyotungwa na Bunge, kwa kuwa mamlaka ya kutunga sheria yanatokana na Katiba, na kwamba kubatilisha sheria ni hatua ya kipekee inayopaswa kuchukuliwa kwa sababu nzito na za lazima.

Amesema kuwa Ibara za 12 na 13 za Katiba zinahakikisha usawa mbele ya sheria, lakini hazikatazi utofautishaji unaofanywa kwa misingi halali na yenye lengo la kijamii au kitaasisi.

Kwa mujibu wa Jaji Mambi, marekebisho ya sheria yalilenga kuoanisha sheria ya Shule ya Sheria na Sheria ya Mawakili, ambayo tayari inatoa nafasi kwa mtu kuomba kusamehewa baadhi ya masharti ya udahili chini ya kifungu cha 16.

Ameeleza kuwa hata mawakili binafsi wenye uzoefu wanaweza kuomba kwa Jaji Mkuu kukubaliwa kama mawakili kwa mujibu wa kifungu hicho cha Sheria ya Mawakili, hivyo hawawezi kudai kuwa wamefungiwa kabisa njia ya kuingia katika taaluma.

Amefafanua kuwa Shule ya Sheria ya Tanzania ilianzishwa ili kutoa mafunzo ya vitendo kwa wahitimu wapya wa sheria, lakini kwa maofisa waandamizi wa umma waliopata uzoefu huo kwa miaka mingi, Bunge liliona kuna msingi wa kuwapatia msamaha wa masharti hayo.

Amehitimisha kuwa mwombaji hakuthibitisha kwa kiwango kinachohitajika kuwa vifungu vinavyolalamikiwa ni vya kibaguzi au vinakiuka Katiba, hivyo kutupilia mbali maombi hayo na kueleza kuwa masharti ya vifungu hivyo ni halali kikatiba.

“Kwa kuzingatia uchambuzi na uchunguzi wangu, naona ombi la mwombaji halina msingi, kwa hiyo nalitupilia mbali,” amehitimisha Jaji Mambi katika uamuzi huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *