Dar es Salaam. Miss Tanzania 2006 na staa wa filamu nchini, Wema Sepetu pamoja na mpenzi wake Whozu ambaye ni mwanamuziki wa Bongofleva, mwishoni mwa wiki iliyopita walitangaza kujaliwa mtoto wa kwanza.
Wema, mshindi wa tuzo za Sinema Zetu International Film Festival Award (SZIFF) 2018, amejaliwa mtoto wa kiume na kumpa jina la Ollie akiwa ni wa kwanza kwake tofauti na ilivyo kwa mwenzake.
Tangazo la kuzaliwa kwa mtoto huyo lilipokelewa kwa furaha kubwa na mashabiki na marafiki wa Wema na Whozu ambao wengi wao wameonyesha hisia zao kupitia mitandao ya kijamii.
Hilo limefanya mtoto huyo kuwa maarufu kwa haraka ambapo ndani ya muda wa wiki moja tu ukurasa wake wa Instagram unaotumia jina la Baby Ollie Oscar tayari ulikuwa umepata wafuasi (followers) zaidi ya 100,000.
Saa chache baada ya tangazo la kuzaliwa kwa mtoto huyo, Whozu alitoa wimbo maalum kwa ajili yake, Namleta (2026) ambao umetayarishwa na S2kizzy ambaye pia ana mchango mkubwa katika safari ya mwanamuziki huyo.
Namleta ni wimbo wa shukrani ambao Whozu anaeleza jinsi alivyokuwa na kiu kubwa ya kuwa na Wema na baadaye akawa na kiu ya mtoto, hivyo sasa anashukuru kwa kupata hitaji lake la moyo wake.
Mwanzoni mwa video ya wimbo huo wameonekana mastaa kama Kajala Masanja, Aunty Ezekiel, Paula na wengineo, wakiwa wamefika hospitalini kumsalimia na kumpongeza Wema au mama Ollie kwa sasa.
Hata hivyo, Whozu si mwanamuziki wa kwanza kutokea kwenye Bongofleva na duniani kwa ujumla kutoa wimbo maalum kwa ajili ya mtoto wake, ipo orodha ndefu ya waliokwisha kufanya hivyo huku nyimbo hizo zikipata mapokezi mazuri.
Rapa wa Marekani, Jay Z baada ya mkewe Beyonce Knowles kujaliwa mtoto wao wa kwanza, Blue Ivy Carter hapo Januari 7, 2012, mwaka huo huo rapa huyo aliachia wimbo kwa ajili ya mwanaye uitwao ‘Glory’ ambao sauti ya mtoto huyo ilisikika ndani yake akiwa amepewa jina la B.I.C.
Wimbo huo uliotolewa siku mbili baada ya Beyonce kujifungua na kuwekwa katika tovuti ya Jay Z, ulipokelewa vizuri hadi kuingia chati za Billboard na kumfanya Blue Ivy kuandika rekodi kama mtu mdogo zaidi kuingia kwenye chati hizo.
Wimbo huu wa Hip Hop uliotayarishwa na kundi la watayarishaji The Neptunes, maneno yake yanaelezea furaha na uzoefu wa kuwa baba kwa mara ya kwanza, huku pia ukizungumzia maumivu waliyopitia baada ya hapo awali ujauzito wa Beyonce kuharibika.
Tukirejea Bongo, mwanamuziki aliyefanya kitu kama hicho miaka ya hivi karibuni ni Marioo baada ya yeye na mpenzi wake, Paula kupata mtoto wao wa kwanza, Princess Amarah ambaye alizaliwa mnamo Mei 2024, na sura yake kuja kuonekana rasmi mtandaoni mwaka mmoja baadaye.
Mwishoni mwa mwaka huo, Marioo aliachia albamu yake ya pili, The God Son (2024) ikiwa na nyimbo 17, ndani ya albamu hii kuna wimbo uitwao ‘My Daughter’ ambao ni maalum kwa ajili ya mtoto wake huyo, Princess Amarah.
Wimbo huo ambao katika video yake ni Paula na mwanaye ndio pekee wameonekana, Marioo anaeleza jinsi anavyompenda na kwamba familia yao yote kuanzia babu na bibi wana furaha kubwa kufuatia ujio wake walioungojea kwa hamu kubwa.
Mbali na Marioo, mwanamuziki mwingine Bongo aliyefanya hivyo ni Jux ila huyu alifanya kabla ya mkewe Priscilla Ojo kutokea Nigeria kujifungua mtoto wao kwanza hapo Agosti 2025 na kumpa jina la Rakeem, mtoto ambaye alizaliwa nchini Canada.
Muda mfupi baada ya kutangaza wanatarajia mtoto, ndipo Jux alitoa wimbo wake, Thank You (2025) ambao katika video yake Priscilla ameonekana akifurahia hatua ya kuelekea kuwa mama kwa mara ya kwanza.
Katika wimbo huo Jux ameeleza hisia zake za kuwa baba kwa mara ya kwanza. Anamuombea mtoto wake baraka kwa Mungu, huku akimueleza kuwa anajivunia kuwa baba yake, na atampenda daima.
Utakumbuka Jux na Priscilla walitangaza wanatarajia kupata mtoto hapo Julai 24, 2025 kupitia Instagram, na kufikia mwishoni mwa Agosti, wakatangaza kuwa wamejaliwa mtoto wa kiume na kumpa jina la Rakeem.