BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema inakaribia kufikia lengo la ununuzi wa dhahabu kabla ya muda waliojiwekea ambapo hadi sasa imefikisha tani 19.3 ndani ya mwaka mmoja na miezi minne. Gavana BoT, Emmanuel Tutuba amesema BoT ilianza kununua dhahabu Oktoba Mosi 2024 na imejiwekea lengo ifikapo Oktoba 2027 iwe imenunua tani 20 za madini hayo.

Tutuba amesema hayo wakati wa mahojiano na kituo cha habari cha Crown ofisini kwake Dodoma hivi karibuni.Amesema Sheria ya BoT Namba Nne ya Mwaka 2006 Kifungu cha Tano inazungumzia majukumu ya benki ambayo mojawapo ni kununua, kuhifadhi, kuwekeza na kutunza fedha za kigeni.

“Ukisoma Kifungu cha 51 kinaelezea aina ya akiba za fedha za kigeni ikiwa ni pamoja na fedha zenyewe, aina ya sarafu mbalimbali. Sisi tunawekeza kwenye Dola ya Marekani, Dola ya Australia, Yuan, Rand, Paundi, pia na kwenye dhahabu kwa sababu kwenye kifungu cha 51 na 52 imeeleza,” alieleza Tutuba.

Amesema BoT inanunua madini hayo kwa sababu kwenye uwekezaji wa masuala ya kifedha na dhahabu kunakuwa na taratibu zake kwa sababu kila aina ya sarafu inakuwa na changamoto zake kwa kuwa inasimamiwa na nchi husika. SOMA: BOT: Uchumi Tanzania kukua 7.2%

Amefafanua kuwa kulingana na mpango wao wa uwekezaji kuna mchanganyiko wa sarafu tofauti tofauti jumla yake lazima itakuwa asilimia 100 kwa hiyo kadri ya uwekezaji unapokuwa mkubwa maana yake unakwenda kufifisha uwiano wa sarafu nyingine.

“Kwenye mkakati huo itakapofikia ukomo ambao uwiano wake umefikia kiwango tunachokihitaji tuna wajibu wa kuendelea kupunguza kwa sababu wakati wananunua walikuwa na malengo tofauti, moja kurasimisha soko la wachimbaji wa ndani na kwa sasa wengi wao wanapenda kuuzia dhahabu zao kupitia Benki Kuu,” alibainisha Gavana wa BoT.

Amesema lengo la pili la kununua madini hayo ni kupata mbadala wa utunzaji wa fedha za kigeni, jingine ni kuwezesha uhimilivu wa thamani ya Shilingi ya Tanzania kwamba unapokuwa na akiba ya fedha za kigeni ikiwa kwenye mfumo wa dhahabu wanaweza kuitumia wakihitaji fedha za kigeni kwa kuuza au kuweka dhamana kwa kiasi cha fedha za kigeni wanazohitaji.

Tutuba amesema Watanzania wengi wana hofu kuhusu uuzaji wa madini hayo kwa kuwa hawafahamu sheria ya BoT na kufahamu namna biashara inavyoenda. Amesema wana Idara ya Usimamizi wa Masoko ya Fedha ambayo inafanya kazi saa 24 kwa sababu BoT kila siku inafanya uwekezaji kwa kuuza na kununua ili kuwezesha wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa kutoka nje wapate dola.

“Wakati tunanunua dhahabu tulikuwa na lengo na tunaona linakaribia kufikiwa na tumejifanyia tathmini kwa mwezi tunapata wastani wa tani 1.1 ya dhahabu hivyo tukaona tukifikia tani 20 kwa miaka mitatu hatutakuwa na changamoto hiyo na hatutaki kuacha kununua kwa sababu ili uendelee kununua lazima uendelee kuuza ili isiathiri uwiano tuliyojiwekea,” alieleza Tutuba. Amesema BoT imepanga kuwa kuuza na kununua dhahabu iwe endelevu hivyo wataendelea kadri wanavyoona inafaa na watanunua ili kuimarisha soko la ndani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *