Kigoma. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi amewataka wananchi wa Kigoma kuishi kwa amani, upendo na mshikamano, akiwasisitiza wasikubali kugawanywa kwa itikadi za vyama.

Amesema Tanzania ni taifa moja isitokee mtu wa chama fulani ampi salamu wa chama kingine. Hiyo si jambo la sahihi kwa sababu wanatakiwa kuishi kwa upendo na kusaidiana katika kila hatua.

Kihongosi ameeleza hayo leo Alhamisi, Februari 19, 2026, akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Matiazo, Kata ya Simbo, Jimbo la Kigoma Kaskazini ambalo linaongozwa na upinzani (ACT Wazalendo).

“Upendo ukatuunganishe, umoja ukatuunganishe, maisha ya upendo ni maisha bora. Vyama vyote tukae pamoja, tule ugali hapo vipi?” amehoji, na kuashiriwa na wananchi waliohudhuria mkutano huo.

Hata hivyo, Kihongosi amesema CCM kitabakia kuwa chama dume, akisema hata upinzani wanalifahamu hilo, ndiyo maana hata katika mkutano huo wamehudhuria.

“Vyama ni majina; vituunganishe, lakini maendeleo ya kweli yataletwa na CCM. Waasisi wa Taifa wameliunganisha Taifa, sasa wasitokee watu wakataka kutugawa kwa itikadi za vyama. Msikubali, pendaneni,” ameeleza Kihongosi.

Akitoa changamoto za Kigoma Kaskazini, mbunge wa Kigoma Kusini Nuru Kashakari ‘Kandahari’ amesema jimbo hilo lina changamoto mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa Soko la Kagunga lililotengewa fedha Sh 1 bilioni, lakini hadi sasa haujatekelezwa.

“Ujenzi wa Soko la Kagunga umechukua muda mrefu licha ya kutengewa fedha na mkandarasi alipewa malipo ya awali; hata hivyo, ameingia mitini. Tunaomba utusaidie maana ni soko la kimkakati kwa wananchi wa Kigoma Kaskazini,” ameeleza Kandahari.

Kandahari amesema changamoto nyingine ni uhaba wa vituo vya afya katika jimbo hilo, pia suala la barabara ya Mkongoro-Mwamgongo hadi Kagunga, ambayo kwa miaka 20 imekuwa ikizungumzwa lakini utekelezaji wake bado haujatimia.

Mbali na hilo, Kandahari amesema miradi ya maji ya Kidahwe, Mkongoro na Mkongonya, akimuomba Kihongosi kuongeza nguvu ili miradi hiyo itekelezwe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *