
Moshi. Mchungaji Godfrey Malisa anayekabiliwa na kesi mbili ikiwemo ya uhaini, ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kuwa anaishi maisha magumu mahabusu na kila siku amekuwa aking’atwa na kunguni.
Amedai kuwa mahabusu ni mahali pagumu ambapo haipiti wiki moja hajatoa machozi kwa kile ambacho anakipitia huko.
Mchungaji Malisa ametoa madai hayo leo Ijumaa Februari 20, 2026 mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Ally Mkama wakati kesi ya makosa ya kimtandao inayomkabili ilipotajwa kwa ajili ya usikilizwaji ambapo ushahidi wa Jamhuri ulitarajiwa kuendelea kutolewa.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 28411/2025, Malisa anatuhumiwa kuchapisha taarifa kwenye mtandao wake wa Youtube, akidai Rais Samia Suluhu Hassan, anatakiwa kujiuzulu kwa kusimamia mauaji ya maelfu ya Watanzania.
Leo mbele ya Hakimu Mkama, Malisa alitoa madai hayo na kuieleza Mahakama kuwa anajua hakuna wanachoweza kufanya ila anataka tu wajue akiwa kama mshtakiwa yuko kwenye kipindi kigumu.
“Naishi jela naliwa na kunguni kila siku hata nikikuonyesha utashangaa, maisha gerezani ni changamoto na yanaumiza sana, haiwezi kupita wiki moja sijatoa machozi kwa kile ninachopitia,” amedai na kuongeza…
“Ni mahali pagumu sana najua hamuwezi kurekebisha hizo tarehe kwa ajili ya kesi, ila nimefurahi Hakimu umeagiza mashahidi waongezwe siku ya kesi.
“Ila ninaporudi gerezani naenda nikiwa na maumivu,ukiniona napanda lori nabebwa naingizwa na nateremshwa,kwa sababu siwezi kupanda. Napitia kipindi kigumu sana,hamna mnachoweza kufanya nataka tu mjue hata mimi kama mshtakiwa niko kwenye kipindi kigumu na chumba kilichopo kule ni watoto wengine wajukuu ni mimi ndiye mtu mzima,nimetaka kusema hilo tu,” ameeleza.
Akijibu hoja hiyo, Hakimu Mkama alimweleza mshtakiwa huyo kuwa anafahamu mazingira ya Magereza na ameshaitembelea mara kadhaa kwani ni miongoni mwa majukumu yake kutembelea mahabusu na wafungwa.
“Bahati nzuri napaelewa magereza tumeshakuja mara nyingi na Machi nitakuja tena,miongoni mwa majukumu yangu ni kutembeleea mahabusu na wafungwa. Nakuhakikishia sisi kama mahakama tulikua tayari kuendelea leo ndio maana nimekaa tangu asubuhi na leo nilipanga kesi yako tu ili upate hatma yako,” amesema.
Hakimu huyo ameeleza kuwa hata katika vikao vyao vya ndani wamekubaliana kumaliza kesi za namna hiyo zinazohusisha matukio ya uchaguzi na baada ya uchaguzi, ili ziishe kwa wakati.
Kabla ya Malisa kutoa madai hayo upande wa Jamhuri uliowakilishwa na Wakili Frank Wambura,aliieleza Mahakama kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kuendelea kusikiliza kwa mashahidi wawili kuanza kutoa ushahidi.
Alidai kuwa mashahidi hao ambao wote ni Askari Polisi, mmoja wao yuko kwenye msafara wa Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba (aliyepo Kilimanjaro kwenye ziara).
“Mwingine wa pili ametumwa Arusha,kwa ajili ya msafara huo wa Waziri Mkuu. Na ndiyo mashahidi ambao tulikuwa tunategemea leo watoe ushahidi, tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya usikilizwaji na hati za wito kwa mashahidi.
Malisa anatetewa na jopo la Mawakili watano wakiongozwa na Deogratias Matata ambao hawakupinga maombi hayo ya Jamhuri.
Kufuatia maombi hayo Hakimu Mkama ameeleza kuwa Mahakama ilifahamishwa kuhusu ugeni huo na kuwa miongoni mwa watakaokuwepo kwenye msafara huo ni mashahidi hao hivyo hiyo ni sababu ya msingi na kukubali ombi la ahirisho.
Hakimu Mkama aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 5, 2026 ambapo aliagiza upande wa Jamhuri kupeleka mashahidi zaidi ya wawili ili kesi hiyo isikilizwe kwa haraka.
Katika kosa la kwanza anadaiwa kutenda Novemba 15,2025 huko Miembeni katika wilaya ya Moshi na alichapisha maneno hayo katika akaunti ya Youtube yenye jina la Godfrey Malisa.
Hati ya mashtaka inanukuu maneno aliyochapisha kuwa alisema,”Samia Suluhu Hassan anatakiwa kujiuzulu mara moja kwa kuwa amekuwa ni Rais aliyesimamia mauaji ya watanzania”.
Upande wa Jamhuri unadsi alichapisha maneno hayo akijua fika kuwa taarifa hizo hazikuwa sahihi na zilikuwa na lengo la kupotosha umma wa watanzania.
Katika kosa la pili,anatuhumiwa kufanya uchochezi kinyume na kifungu cha 35 cha Kanuni ya Adhaby sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Maelezo ya kosa ni kuwa Novemba 15,2025 huko Miembeni wilaya ya Moshi, anadaiwa kuchochea umma wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutenda kosa la jinai ambalo ni kufanya mkusanyiko usio halali kinyume cha sheria
Kesi ya uhaini
Mbali na kesi hiyo, mchungaji Malisa anakabiliwa na kesi ya uhaini chini ya kifungu 39(2)(d) cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama kilivyofanyiwa marejeo na Bunge mwaka 2023, akituhumiwa kuhamasisha mkusanyiko usio halali hapa Tanzania.
Februari 10, 2025 mchungaji Malisa ambaye ni mwanazuoni mwenye shahada ya Uzamivu (PhD), alifukuzwa uanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya kupinga maamuzi ya mkutano mkuu wa CCM uliomteua Rais Samia kuwa mgombea urais.
Maamuzi ya kumfukuza uanachama yalitangazwa na Katibu wa CCM mkoa wa Kilimanjaro, Merce Mollel, akiegemea maamuzi ya Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Kilimanjaro iliyomuondolea sifa ya kuendelea kuwa mwanachama.
“Malisa amefukuzwa kutokana na kukosa sifa za kuendelea kuwa mwanachama kwa sababu mara kwa mara amekuwa akibeza maamuzi halali yaliyofanywa na mkutano mkuu wa CCM taifa uliofanyika Januari 19,2025,”alieleza Mollel.
Katibu huyo alinukuliwa akidai Malisa amekuwa akitoa matamko ambayo hayaleti umoja na mshikamano ndani ya chama na nchi kutokana na kudai mkutano huo uliomteua Samia kuwa mgombea pekee ulivunja katiba jambo ambalo si la kweli.
Pamoja na kufukuzwa uanachama, bado aliendelea kupinga uteuzi huo kwa kujaribu kufungua kesi mahakamani ambazo hata hivyo hakufanikiwa, ambapo alihamia katika mitandao ya kijamii akiendelea kupinga uteuzi huo.