SERIKALI imepiga marufuku matumizi ya mitandao binafsi zikiwemo baruapepe, WhatsApp, Instagram, You Tube, Facebook kutuma nyaraka na taarifa za serikali.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete ametangaza amri hiyo wakati akifunga kikaokazi cha sita cha Serikali Mtandao kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) jijini Arusha jana. Ridhiwani aliwaomba watumishi wote wa umma kuendelea kuiamini mifumo ya mawasiliano serikalini ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa sababu ni imara, salama na inayoleta tija kwa mawasiliano yote ya serikali.
Amesema kuna watumishi wa umma ambao bado wanatumia njia na mitandao binafsi kutuma na kupokea taarifa na nyaraka mbalimbali za serikali, na kusisitiza kuwa hayo ni matumizi mabaya ya mifumo ya mawasiliano serikalini.
“Ni marufuku kuanzia leo kwa watumishi wote wa umma kutumia mitandao isiyo rasmi kutuma na kupokea nyaraka za serikali, kwa sababu hilo ni jambo la hatari na linasababisha nyaraka za serikali kuvuja na kuonekana mitaani,” alisema Ridhiwani.
Ameeleza kusikitishwa na kitendo cha watumishi wa umma kuendelea kuteswa na mikopo ya kausha damu wakati utaratibu wote wa mikopo salama unapatikana katika mifumo ya mawasiliano serikalini. Amesema ni jambo la ajabu kuona watumishi wakilalamikia mikopo ya kausha damu, wakati serikali imewawekea mifumo inayowahakikishia kutotapeliwa na kupata mikopo inayofuata taratibu za ukopeshaji zinazotambuliwa na serikali.
“Watumishi wanatakiwa kutumia mifumo ya Tehama ambayo inayaleta mashirika yote pamoja na taasisi za fedha pamoja kuomba mikopo, kwa sababu ndio sehemu wanaweza kupata mikopo bila usumbufu wowote na kwa riba nafuu,” alisema Ridhiwani.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Benedict Ndomba alisema kikaokazi hicho kimeshirikisha wadau zaidi ya 1,300 kutoka sekta za umma na binafsi na kwamba mada 14 ziliwasilishwa. Ndomba alisema kutokana na taasisi mbalimbali za umma kutekeleza vyema miradi ya Tehama, eGA imeamua kuwapa tuzo ili iwe motisha kwao waendelee kufanya vizuri pamoja na kukuza weledi katika utendaji.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro amesema Tanzania imepata mafanikio Afrika katika eneo la Serikali Mtandao na kwamba kwa dunia ya leo, ni lazima kuwekeza katika Tehama ili Tanzania isonge mbele.
Dk Ndumbaro amesema kutokana na kazi nzuri ya eGA, kamati ya bunge inatambua mafanikio ya taifa na kwamba eGA imefanikiwa kuunganisha mifumo ya mawasiliano serikalini. “Bunge ni mnufaika mzuri wa Serikali Mtandao, kwa sababu halitumii tena karatasi katika kuwasiliana na badala yake kwa sasa kila kitu kinafanyika mtandaoni,” alisema Dk Ndumbaro.
Aidha amesema kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na eGA, muda mwingi wa wabunge umeokolewa na kwamba gharama kubwa iliyokuwa ikitumiwa na bunge kuchapa karatasi sasa imeokolewa. SOMA: Mastaa, mikopo mitandaoni vinara malalamiko taarifa binafsi
