Arusha. Hatimaye mwili wa mfanyabiashara maarufu wa madini jijini Arusha, Abdilah Mussa maarufu kama ‘Banjoo’ (54), umezikwa huku familia yake ikiomba Serikali kusaka watuhumiwa waliompora uhai wake kinyume cha sheria.

Mwili wa Banjoo umezikwa jioni ya leo, Februari 20, 2026, katika makaburi ya familia yaliyopo eneo la Moivo, mkoani Arusha.

Marehemu, ambaye alikuwa mkazi wa Sanawari jijini Arusha, anadaiwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana Februari 12, 2026, chini ya jengo la ghorofa 10 linalomilikiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, alipokuwa akitoka mazoezini (gym).

Baada ya tukio hilo, hakujulikana alipo hadi Februari 18, 2026, mwili wake ulipokutwa kando ya barabara katika eneo la Bereko, Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma.

Taarifa zinaeleza kuwa mwili huo ulikuwa na majeraha makubwa kichwani, mikono ikiwa imevunjwa na macho yakiwa yametobolewa.

Akizungumza wakati wa mazishi, mke wa marehemu, Jamilla Mohamed amesema familia imepokea taarifa za kifo hicho kwa mshtuko mkubwa, huku wakisikitishwa na hali ya mwili wake ulivyokutwa.

“Kiukweli mume wangu amedhulumiwa sana maisha yake. Hata kama alifanya kosa lolote, hakustahili kuuawa kwa mateso ya namna hii. Ilipaswa afikishwe kwenye vyombo vya usalama na kuchukuliwa hatua za kisheria,” amesema mjane huyo.

“Kikubwa hatuoni mwelekeo wa haki ya mume wangu kupatikana naomba Rais Samia Suluhu Hassan aingilie suala hili ili haki ya mume wangu iweze kupatikana, maana sisi kama familia hatuna cha kufanya,” amesema.

Akizungumzia siku ya tukio, Jamilla amesema jioni ya Alhamisi, Februari 12, 2026, mume wake aliaga kama ilivyokuwa kawaida yake kuwa anaelekea kufanya mazoezi katika jengo la Ngorongoro.

Amesema ilipofika majira ya saa mbili usiku bila kurejea nyumbani, familia ilianza kupata wasiwasi na kuingiwa na mashaka kuhusu usalama wake.

“Hana kawaida ya kuchelewa kurudi maana anaingia swala ya jioni,  hivyo tulianza kumpigia simu zake bila kupokelewa na nyingine ilikuwa haiiti kabisa imezimwa.

“Tuliamua kusubiri tukidhani labda amepata dharura lakini hadi asubuhi kukawa kimya kitendo kilichotia mashaka zaidi maana hana desturi ya kulala nje bila taarifa,” amesema.

Amesema kuwa siku iliyofuata, Ijumaa, waliamua kwenda Kituo cha Polisi kutoa taarifa ya kupotea kwake, ambapo waliambiwa wasubiri kwa saa 24 kama utaratibu wa awali wa ufuatiliaji.

Aidha, amesema waliendelea kupiga simu yake, ambayo moja ya namba zake ilikuwa bado ikiita, huku wakijaribu kumtafuta kupitia ndugu, jamaa na marafiki, lakini jitihada hizo hazikuzaa matunda.

“Siku ya nne tuliamua kutoa taarifa kwenye vyombo vya habari na kusambaza picha yake ndio tukapigiwa simu kutoka Dodoma kuwa kuna mwili uliokotwa pembeni ya barabara eneo la Bereko tukautambue.

“Watoto waliamua kufunga safari hadi Kondoa kutambua mwili huo na bahati mbaya kweli ukawa ni mwili wa baba yao,” amesema.

Akizungumzia kama mume wake alikuwa na ugomvi na mtu yoyote, Jamilla amesema kuwa wiki iliyoisha kabla ya kutekwa aliitwa Polisi na kuhojiwa lakini aliachiwa

“Mwisho wa wiki aliniambia ameitwa Polisi kuhojiwa bila kunieleza sababu ya kuitwa na alihudhuria hadi siku hiyo ya mwisho wa wiki aliporudi nilimuuliza kulikoni, akasema amehojiwa vitu ambavyo haelewi na baada ya kujieleza aliachiwa na kesi hakuna,” amesema.

Amesema mbali na kuitwa Polisi kwa ajili ya mahojiano, mumewe hakuwa na ugomvi na mtu yeyote, akisisitiza kuwa hadi anapoteza maisha yake hakuwa na mzozo unaojulikana.

Kifo cha Banjoo, mbali na kuzua hofu na majonzi, pia kimeibua mashaka miongoni mwa wafanyabiashara wa madini jijini Arusha, huku kikizua maswali kuhusu kutopatikana kwa watuhumiwa hadi sasa.

Leo, Februari 20, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo, akizungumza kwa njia ya simu, amesema kwa sasa hawezi kuweka taarifa zozote hadharani hadi pale upelelezi utakapokamilika.

“Upelelezi unaendelea tutawapa taarifa kwa hatua za awali tulipofikia tukikamilisha, kikubwa tunaomba mtu yoyote anayeweza kusaidia kupatikana kwa watuhumiwa aje kutoa ushirikiano,” amesema na alipoulizwa kama kuna watu wanashikiliwa alikata simu.

Hata hivyo, hadi mfanyabiashara huyo alipokuwa akizikwa, maswali na minong’ono imeendelea kuongezeka kuhusu kutokamatwa kwa wahusika, ilhali jengo hilo linadaiwa kuwa na ulinzi mkali pamoja na kamera za usalama (CCTV) zinazofanya kazi muda wote.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, upande wa mbele wa jengo hilo pekee una kamera tatu; moja upande wa kushoto, nyingine upande wa kulia na ya tatu ikiwa katikati karibu na lango kuu la kuingilia. Kamera hizo zinadaiwa kuwa zinalenga moja kwa moja waingiaji, watokaji na watu wanaozunguka eneo hilo.

Mbali na kamera hizo, jengo hilo pia hulindwa na askari waliopo pande za kushoto na kulia, pamoja na walinzi waliopo katika eneo la mapokezi wakiwa na silaha za moto kwa ajili ya kulinda usalama wa mali na ofisi za wafanyabiashara waliomo ndani ya jengo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *